NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kusogeza huduma zake karibu na jamii kwa kufanya zoezi maalumu la uchunguzi na matibabu ya moyo kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma wanaohudhuria kikao kazi kinachofanyia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilichopo jijini Arusha.
Kikao kazi hicho kimeandaliwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuwakutanisha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma wapatao 600.
Katika zoezi hilo viongozi hao wanapimwa shinikizo la damu, kiwango cha sukari mwilini, vipimo vya maabara, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo huku wakipewa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuishi maisha yenye afya bora ya moyo.
Akizungumzia kuhusu zoezi hilo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema lengo la huduma hiyo ni kutoa elimu na hamasa kwa viongozi juu ya umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ili kuepusha madhara ya kuchelewa kugundua magonjwa ya moyo.
“Magonjwa ya moyo hayana dalili za haraka, mara nyingi yanapogundulika yanakuwa yamefika hatua kubwa. Ndiyo maana tunahimiza watu wote wakiwemo viongozi kupima afya za mioyo yao mapema”, alisisitiza Dkt. Mwinchete
Baadhi ya viongozi waliopata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo walieleza kufurahishwa na huduma hiyo na kupongeza ubunifu wa JKCI wa kusogeza huduma nje ya kuta za hospitali. Walisema hatua hiyo ni ya mfano kwa taasisi nyingine za umma na binafsi, kwani afya njema ya kiongozi ni chachu ya kuimarisha ufanisi katika utendaji wa majukumu ya kila siku.
“Ninashukuru kwa huduma niliyoipata, wiki iliyopita mlikuwa Shinyanga lakini nilikosa kupata huduma ya upimaji kwani nilikuwa nje ya mkoa. Baada ya kuwaona mko katika mkutano huu nikaona nitumie nafasi hii vizuri kupima afya ya moyo wangU, nimepima na kupata elimu ya lishe bora ambayo itanisaidia kujua jinsi gani nitautunza moyo wangu”, alisema Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola.
“Huduma zenu ni nzuri na za kiwango cha kimataifa, katika mkutano huu mpewa zawadi ya mshindi wa kwanza katika uboreshaji wa utoaji huduma za afya, muendelee kusonga mbele msirudi nyuma jambo la muhimu ni kutangaza huduma mnazozitoa ili ziwafikie watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi”, alisema Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi Balozi Salome Sijaona.