NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa kiwango cha uchangiaji na ulipaji wa kodi katika Michezo ya kubahatisha umeongezeka kutoka Sh.Bilioni 131.99 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Bilioni 260.1 kwa mwaka 2024/25
Ongezeko hilo la kiasi cha fedha linatajwa kufikia asilimia 97.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Agosti 12, 2025 jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa Huduma wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Daniel Ole Sumayan kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) katika Mkutano kati ya Wahariri na Waandishi wa Habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kueleza mafanikio ya Bodi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan madarakani.
Amesema mafanikio anayataja kama mchango wa Bodi hiyo katika uchumi ambapo pamoja na kuchangia kodi pia imefanikiwa kutoa ajira 30,000 ambazo ni rasmi na zisizo rasmi.
Aidha Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na zaidi ya Sh.Bilioni 66.7 kuingizwa nchini kutoka kwa wawekezaji wapya kwa kipindi cha miaka miwili.
Pia ameeleza kuwa Bodi hiyo imewezesha kukusanya kwa fedha ndogo ndogo na kuifanya kuwa mitaji mikubwa iwezayo kuwekeza jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangamsha uchumi wetu.
Fauka ya hayo ,Ole Sumayan amebainisha kuwa Bodi imewezesha kuchangia Sh.Bilioni .53.8 kwaajili ya kuendeleza michezo nchini
Akizungumza juu ya kero ya vijana kuharibikiwa na Michezo ya kubashiri Ole Semayan amesisitiza vijana wanapaswa kufahamu kwamba kubashiri sio ajira bali ni burudani hivyo basi vijana wanapaswa kuondokana na dhana hiyo potofu na badala yake kufanya kazi.
“Michezo ya kubahatisha ni sehemu nyingine ambayo imeongeza wigo wa burudani, kwa hiyo inapaswa kuwa sehemu ya burudani kwa wanaocheza na si kazi, hii ni bahati, kwani kwenye michezo hii hakuna ufundi wowote wa kucheza.” amekazia Mkurugenzi huyo
Kuhusu malalamiko juu ya raia wa kigeni kuweka mashine za michezo ya kamari kila kona za mitaa ,amesema kuna ufuatiliaji mkubwa wa suala hilo na iwapo mtu atabainika kufanya makosa kwa kutofuata utaratibu uliowekwa huchukuliwa hatua ikiwemo faini ,kifungo au vyote viwili.