NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wamesaini makubaliano ya ushirikiano kwa lengo la kulinda kazi za sanaa nchini, kupitia usajili wa kazi na miradi ya ubunifu pamoja na kutumia haki za ubunifu kama mtaji wa maendeleo.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Agosti 12, 2025, jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk.Kedmon Mapana na kushuhudiwa Waandishi wa Habari.
Akizungumza katika hafla hiyo,Nyaisa amesema makubaliano hayo yanalenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu kisheria na kiuendeshaji kupitia kubadilishana taarifa kwa njia za TEHAMA, ili kurahisisha utoaji huduma, kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa wasanii kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara na kulinda kazi zao.
Ameeleza kuwa makubaliano hayo pia yatawezesha urasimishaji wa shughuli za burudani, ikiwemo kumbi za muziki na burudani (night clubs), kwa kuzingatia vigezo vya kibunifu na kibiashara, sambamba na kusukuma mbele kazi za sanaa za asili na utamaduni wa Kitanzania ili zipate nafasi katika soko la ndani na kufikia viwango vya kimataifa.
“Ni ukweli usiopingika kuwa sekta ya ubunifu na sanaa inakua kwa kasi, na inazidi kuwa nyenzo muhimu ya ajira, utambulisho wa taifa na chanzo cha mapato. Ni jukumu letu kama taasisi kuhakikisha tunaunda mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji ili kusaidia ukuaji huo. Hivyo, utiaji saini wa makubaliano haya ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea ndoto hiyo,” amesema Nyaisa.
Kwa upande wake, Dk. Mapana amebainisha kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria kwani urasimishaji wa kazi za sanaa kupitia usajili wa alama zinazowatambulisha wasanii kabla ya kuziingiza sokoni, utawapa ulinzi unaowezesha ukuaji wao wa kiuchumi.
“Sekta inayoongoza katika ukuaji wa uchumi ni Sekta ya Sanaa na Burudani kwa asilimia 17. Ukuaji huu unatokana na kazi kubwa ya wasanii, na kupitia urasimishaji wa kazi zao watapata elimu ya bure ya kisheria na fursa za mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni, ili waweze kukua kiuchumi,” amesema Dk. Mapana.
Aidha, ametoa wito kwa wanamuziki wanaotarajia kushiriki katika Tuzo za Kitaifa za Muziki Tanzania (TMA) zitakazofanyika Septemba 2025, kuhakikisha wanasajili alama zinazowatambulisha ili kulinda haki zao za kisanaa.
Wito huo pia unawahusu washiriki wa mashindano ya ulimbwende mwaka 2027, ambayo Tanzania itaandaa.