*WANAHABARI 16 WANG’ARA
*WAMO MANYERERE,KIKEKE ,MKOTYA,MCHANGE,AKILIMALI,MIHANJI,MSOWOYA,MAMMY BABY, NKAMIA,MURUSURI,SILEMU,MUHUZA,IBWE,DAUDA,KIJA NA MAKONGO
NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
KAMATI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imetangaza rasmi uteuzi wa awali wa wanachama wa chama hicho ambao watashiriki katika zoezi la kura za maoni katika nafasi ya ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi.
Majina ya wanachama hao yametangazwa leo Julai 29,2025 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Makalla amesema katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Julai 28, 2025 jijini Dodoma pamoja na mambo mengine, imepitia na kujadili majina ya wanachama wake walioomba kupendekezwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Amesema kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi wa majina ya wanachama ambao watapigiwa kura za maoni kwa mujibu wa Kanuni na Kalenda za chama hicho.
Hata hivyo Demokrasia imechambua taarifa hiyo na kukuletea majina ya wanasiasa maarufu , wafanyabiashara pamoja na wasanii waliofyekwa katika mchakato huo wa awali.
Kwa upande wa wanasiasa waliofyekwa katika mchakato huo wa awali ni aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini, Mrisho Gambo ambaye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake.
Katika jimbo hilo la Arusha Mjini waliofanikiwa kuteuliwa na Kamati Kuu ili kwenda katika kura za maoni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ,Ally Said , Hussein Gonga, Aminata Teule, Mustapha Nassoro pamoja na Ruhembo Kishugua.
Wengine waliotemwa katika mchakato huo wa kura za maoni ni aliyekuwa mbunge wa Bumbuli, January Makamba.
Jina la Makamba halijaweza kurudi huku majina yaliyopenya ni Hidaya Kilima, Zahoro Hanuna, Ramadhan Singano, Rashid Kilua, Silas Shehemba na John Kilima.
Itakumbukwa kuwa Makamba amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri kuanzia Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, ya tano iliyoongozwa na hayati John Magufuli hadi sita ya Samia Suluhu Hassan.
Mwanasiasa huyo mbaye amebobea katika uchambuzi na usuluhishi wa migogoro aliingia bungeni kuanzia mwaka 2010, amewahi kuwa msaidizi wa Rais wa awamu nne, Jakaya Kikwete kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.
Wakati anawania Jimbo la Bumbuli, Makamba alishinda kwa kupata kura 14,612 dhidi ya mpinzani wake William Shelukindo aliyepata 1,700 ambaye pia alikuwa akitetea jimbo hilo kwa awamu nyingine.
Hata hivyo Kamati Kuu hiyo pia imepitisha majina saba ambao wataingia katika mchakato wa kura za maoni kuwania ubunge jimbo la Kisesa mkoani Simiyu huku aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Luhaga Mpina jina lake likikosekana.
Katika jimbo hilo,waliopitishwa ni saba na ndio watasubiria kura za wajumbe Agosti 4, mwaka huu ili kuamua nani ateuliwe na chama hicho kugombea ubunge wa Kisesa.
Watiania hao walioteuliwa ni Lusingu Makanda, Silinde Mhachile, Joel Mboyi, Madili Sakumi, Godfrey Mbuga, Elias Mambembela na Gambamala Michael Luchuga.
Mpina ameliongoza jimbo hilo tangu mwaka 2005 na amewahi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na baadaye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020.
Aidha Kamati hiyo imewateua Wagombea sita kugombea Ubunge Jimbo la Arumeru Magharibi akiwemo Dk. Lukumai, Noah Mollel, Noel Severe, Ester Mollel, Herietha Temu, Luteni Kanali Meidin.Hata hivyo chama hicho hakijarudisha jina la Ole Sabaya.
Wengine walioenguliwa ni mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Babati mjini, Paulina Gekul.
Gekul, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini zikiwemo nafasi za Naibu Waziri wa Mifugo,Naibu Waziri wa katiba na sheria, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, alichukua fomu ya kugombea mapema mwezi huu akiomba ridhaa ya chama chake kuendelea kuwakilisha wananchi wa Babati Mjini.
Kutokuwepo kwa jina la Gekul katika orodha ya wagombea wa CCM kunafungua ukurasa mpya wa siasa katika Jimbo la Babati Mjini, ambapo sasa wagombea wapya ndio watakaowania kupitishwa na chama kupitia kura za maoni zinazotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Wafanyabiashara na watu maarufu waliotemwa
Kwa upande wa wafanyabiashara waliotemwa katika mchakao huo ni Freddy Ngajilo maarufu Vunjabei.
Vunjabei ameshindwa kupita kwenye mchujo wa awali uliofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika kuwapata wawakilishi jimbo la Kalenga.
Akitangaza matokeo ya waliofanikiwa kupita katika hatua ya awali, Makalla amewataja wagombea waliotia nia Jimbo la Kalenga na kupata nafasi ya kuwakilisha Jimbo hilo kwenye kura za maoni ni, Jackson Kiswaga, Mussa Mdede, Grace Tendega na Thomasy Nyaulingo.
Mwingine aliyetemwa ni Rais wa Yanga, Injinia Said Hersi ambaye alitia nia ya kugombea ubunge jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Waliopita katika jimbo hilo ni Ponela Matei, Habib Mchange, Allan Sanga, Henjelewe, Ally Mandai na Francis Elias.
Hersi anaungana na Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku ambaye naye jina lake halijaweza kurudishwa katika jimbo la Mvomero.
Majina ambayo Kamati Kuu ya CCM imeyarudisha na watachuana katika kura za maoni ili mmoja kupata nafasi ya kugombea katika jimbo hilo ni Suleiman Ahmed, Stoys Simbachawene, Yusuph Makunja, Jonan Van, Sara Msafiri, Bright Fidelis; Adam Joseph na Prosper Remmy.
Waliopenya
Kamati huu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimewateua Wagombea wanne kugombea Ubunge Jimbo la Mtama Mkoani Lindi akiwemo mbunge aliyemaliza muda wake Nape Nnauye.
Wengine walioteuliwa na chama hicho ni Jemedari Kazumari, Jabir Chilumba na Meta Nahonyo.
Aidha chama hicho kimewateua watiania saba kuingia katika mchakato wa kura za maoni kuwania Ubunge jimbo la Chemba pia kimeteua majina manne ya watiania jimbo la Kondoa mjini huku Kondoa vijijini majina matano nayo yakirudi.
Makalla amewataja Kunti Majala, Amina Bakari, Hamis Mkotya, Juma Nkamia, Omary Puto na Francis Julius kuwa ndiyo watiania wa ubunge wa Chemba waliopendekezwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwenda hatua ya kupigiwa kura za maoni.
Katika Jimbo la Kondoa Mjini walioteuliwa ni Ally Makoa, Mariam Mzuzuri, Ally Juma na Dk Athuman Nchana huku watiania watano wameteuliwa katika Jimbo la Kondoa Vijijini ni Ashatu Kijaji, Said Mnyeke, Hassan Lubuga, Juma Shaaban na Hans Kida.
Kinondoni
Kwa upande wa Kinondoni Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imewateua watiania wanane kuingia kwenye mchakato wa kura za maoni kuwania ubunge wa Jimbo hilo.
Makalla amewataja watiania hao kuwa ni Wilfred Nyamwija, Abbas Tarimba, Idd Mohamed, Michael Wambura, Jerusa Kitoto, Julieth Lushuli, Wan’goto Salum pamoja na Zena Kiputiputi.
Katika hatua nyingine majina ya wanahabari 16 yameonekana kung’ara na kupitishwa katika mchakato kwa majimboni na Viti Maalumu.
Wanahabari hao ni Jackton Manyerere,Salim Kikeke,Baruani Muhuza,Juma Nkamia,Hamis Mkotya,Jackline Silemu,Hashim Ibwe,Habib Mchange,Derek Murusuri ,Angelina Akilimali,Shaffih Dauda na Cosmas Makongo.
Wengine ni Tumaini Msowoya,Jane Mihanji, Mkuwe Isale na Kijah Yunus