NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango ameungana na waumini pamoja na viongozi mbalimbali wa Kanisa katoliki kushiriki katika Misa Takatifu ya Upadirisho pamoja na Ufunguzi wa Mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma.
Misa hiyo Takatifu imefanyika katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska – Kiwanja cha Ndege na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya.
Askofu Kinyaiya amewasisitiza waumini kujitokeza katika kupiga kura kuchagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu watakaowatumikia kwa miaka mitano ijayo. Pia ametoa rai ya matumizi sahihi ya akili mnemba (AI) ili kuepusha maovu na udanganyifu katika jamii.
Jumla ya Mashemasi watatu wamepata daraja la Upadre katika Misa hiyo ambao ni Padre Joseph Ibrahim, Padre Sajilo Mark pamoja Padre Damian Mtanduzi.
Aidha Misa hiyo imeambatana na uwekaji wa Jiwe la Msingi ujenzi wa jengo la Katekesi (Jengo la kufundishia dini) lililopo katika Parokia hiyo ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska – Kiwanja cha Ndege.