* YASAMBAZA MBOLEA YENYE THAMANI YA SH.BILIONI 708.6
*NI KWA WAKULIMA WA MAZAO YOTE NCHINI
NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WADAU wa Tasnia ya mbolea wameipongeza serikali kwa utekelezaji wake madhubuti wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea ambao katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita umechochea matumizi ya pembejeo hiyo katika sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.
Serikali ya Rais wa Awamu Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan, ilizindua utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya mbolea katika maadhimisho ya sherehe za wakulima zilizofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya mwaka 2022/2023 ili kukubaliana na ongezeko la bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.
Akiwasilisha bajeti ya 2025/26, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema katika miaka mitatu ya 2022/23 hadi 2024/25 serikali imesambaza mbolea ya ruzuku yenye jumla ya tani 1,454,974,721 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 708.6 kwa wakulima wa mazao yote nchini.
Alisema utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la matumizi ya mbolea kutoka
tani 363,599 mwaka 2021/22 hadi tani 848,884 mwaka 2023/24.
Wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni ya ETG Agri Input Tanzania wameunga mkono thathmini hiyo ambapo viongozi wake wamesema ruzuku ya mbolea imeleta maboresho makubwa katika upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini.
“Mbolea imekuwa ikipatikana kwa bei nafuu ukilinganisha na bei ya soko. Hali hii imeongeza uwezo wa wakulima kununua mbolea kwa wakati.
Tangu kuanza kwa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea, Kampuni ya ETG imesambaza tani 300,000 za aina mbalimbali za mbolea kupitia mtandao wake wa maghala, maduka na wafanyabiashara.
“Kwa msimu ujao, tumejipanga kuendelea kushiriki kikamilifu katika kusambaza mbolea kupitia mfumo wa pembejeo za Ruzuku kwa kuongeza idadi ya vituo vya
mauzo, kushirikiana na wafanyabiashara (agrodealers) na kuongeza ufanisi wa usambazaji kupitia mfumo wa Last Mile Delivery na tunaishukuru sana serikali kwa kuendelea kulipa ruzuku hii.” taarifa ya ETG inaeleza.
“Pia tumejipanga kuwa na mbolea ya kutosha kabla ya kuanza kwa msimu ili kuepuka ucheleweshaji wa bidhaa hiyo kwa wakulima. Hivi sasa tuna meli tatu bandarini zinazosubiri kupakuliwa tayari kwa ajili ya kuwasambazia wakulima kwa ajili ya msimu mpya wa ruzuku wa 2025/26.”
Taarifa inaendelea kueleza kuwa “Mpango huu (wa ruzuku) umeongeza wigo wa biashara kwa kampuni yetu kwa kuwafikia wakulima wadogo vijijini pia tumepata nafasi ya kushirikiana moja kwa moja na serikali, kuongeza uaminifu wa kampuni yetu sokoni na kuchangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kuwawezesha wakulima kutumia pembejeo bora kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Minjingu Mine and Fertiliser Company iliyoko mkoani Manyara, Hans Tosky, amesema kwa ujumla ulipaji wa fedha za ruzuku umekuwa wa kuridhisha kwa vile kampuni yake imekuwa ikipokea malipo wakati wote.
Ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo na kuahidi kwamba kampuni yake imehamasika kuendelea kuwahudumia wakulima nchini.
Kuhusu maandalizi ya msimu ujao, Tosky amesema “Tumejipanga kuwahudumia wakulima kwa kuzingatia kwamba viwanda vya ndani vina fursa nyingi ya kuweza kujitanua na kupata masoko ndani na nje ya nchi.”
“Mbolea zinazozalishwa na kiwanda chetu zimeshafahamika na kukubalika kwa wakulima na hivyo kampuni inatarajia kuzifikisha mbolea hizo kwa wakulima mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo,” Tosky anaeleza.
Amesema, Mpango wa Ruzuku ya Mbolea umemletea mkulima wa Tanzania ahueni ya makali ya bei ya bidhaa hiyo na upatikanaji wake ikilinganishwa na siku za nyuma.
Jambo jingine la kutia moyo, kwa mujibu wa Tosky, ni kwamba mbolea zinazozalishwa nchini zimepata nafasi kubwa katika ushindani kwenye soko na zile zinazoagizwa kutoka nje.
Nayo Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imeeleza katika taarifa yake kwamba Mpango wa Ruzuku ya Mbolea umesaidia sana kuleta ustahimilivu wa bei na kuongeza matumizi yake.
Kampuni imesema upatikanaji wa mbolea kwa wakati na matumizi yake sahihi umechochea ongezeko la tija ya mazao mbalimbali nchini.
“Mpango huu umewezesha utambuzi wa wakulima na maeneo yao. Umepunguza mwanya wa utoroshaji wa mbolea na matumizi mabaya ya fedha za serikali,” taarifa ya TFC imesisitiza.
Kuanzia mwaka 2022/23, TFC ilisambaza tani 4,500 za mbolea zenye thamani ya shilingi bilioni 8.9, mwaka 2023/24 tani 29,133.25 zenye thamani ya Sh Bilioni46.5 na mwaka 2024/25 tani 54,500 zenye thamani ya shilingi bilioni 81.5.
Kampuni ya Mbolea inakiri kunufaika kwa kuongeza mauzo na mtajiwa usambazaji wa mbolea kwa wakulima nchini kupitia ruzuku.
“Serikali iendelee kuweka ruzuku kwenye mbolea, ikiwezekana kwenye mbolea zote,” TFC inasisitiza katika taarifa yake.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Itracom Nduwimana Nazaire ameeleza kuwa, kama wazalishaji wa ndani kwa msimu wa kilimo 2024/2025 Mbolea za FOMI zilipatiwa ruzuku kubwa na bei ya mkulima ikawa nafuu na hivyo kuwawezesha kumudu gharama za mbolea na kuongeza tija ya uzalishaji.
Amekiri, uwepo wa mpango wa ruzuku kumechangia sana wakulima kupata mbolea Za FOMI kwa bei na kuahidi kuendelea kushiriki kwenye usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa msimu ujao wa 2025/2026 ambapo wanatarajia kusambaza kiasi cha tani laki tano.