NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKUU wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Meja Jenerali Shaban Mani amesema kuwa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) kina mpango wa kuendelea na kozi zitakazosaidia na kuwajengea uwezo watanzania wote wakiwemo wanajeshi, polisi na raia wa kawaida katika kwenda kushiriki kulinda amani ndani na nje ya nchi.
Meja Jenerali Mani ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya ulinzi wa amani yaliyotolewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo hicho cha TPTC chini ya ufadhili wa serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNPD).
Lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa na kuwawezesha raia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na waledi wanapokuwa kwenye jukumu ya ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo, Meja Jenerali Mani amesema chuo hicho pia kina mpango wa kuwa kituo kikubwa cha kikanda katika kufundisha watu kwenda kulinda amani wakiwemo wanajeshi, polisi na raia wa kawaida katika.
Amesema kwenye kulinda amani raia wa kawaida wana nafasi muhimu hivyo kupitia Serikali ya Japan na UNDP wameweza kuandaa kozi yao ambayo inashirikisha raia katika ulinzi wa amani.
“Kozi hii ya ushirikishwaji wa raia kwa JWTZ na Tanzania inatupa uwezo wa kujijenga zaidi kwa kuhakikisha kwamba kila tunapokwenda kwenye mission ya kulinda amani tunakuwa tumekamilika katika Idara zote kwa kuwa na watu wenye weledi kwenye kufanya kazi zao kulingana na taratibu na sheria zinazotaka raia aende kufanya,” amesema na kuongeza
“Kozi hii itakijengea uwezo Chuo cha TPTC kuwa kituo kikubwa katika ukanda cha kufundisha watu wake kwenda kulinda amani katika nchi mbalimbali,” amesema
Naye Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, John Rutere amesema shirika hilo litaendelea kufanya kazi na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha raia wanapata mafunzo hayo ya ulinzi wa amani.
Amesema kozi hiyo iliyotolewa itawafanya wale wote waliopata kupata ujuzi wa kutosha na kuifanya Tanzania kuwa na walinda amani wengi na kuifanya nchi iongeze ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
“Kozi hii ni ya kwanza lakini siyo ya mwisho na itaisaidia Tanzania kupata walinda amani wengi, tutaendelea kuongea na mashirika mengine tunaoshirikiana nao kuona kama tutaendelea na mafunzo haya na kuwafungulia watu kutoka nchi zingine kuja kujifunza,” amesema
Naye Mwakilishi wa Ubalozi wa Japan, Nomura Hiroyuki amesema mafunzo hayo ya anapaswa kuwa endelevu na ndio mpango uliopo sasa.
Kwa upande wake mmoja wa watu waliopata mafunzo hayo ambaye ni Ofisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nice Munissy amesema moja ya majukumu waliofundisha ni kuhakikisha wanatekeleza sera ya mambo ya Nje ikiwemo kuimarisha ulinzi wa amani ambayo inagusa maslahi ya watu wote
“Mimi ni mshiriki wa mafunzo haya ambayo yamekuwa na tija sana hapa kwetu, nifundishwa tunawezaje kushirikiana na wenzetu tunapokuwa katika mission za kulinda amani,” amesema
Amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa ikishiriki michakato ya kusaidia nchi nyingine kupata uhuru wao, kusuluhisha migogoro na kuleta upatanishi pamoja na kusaidia nchi zisizo na amani.
Kwa upande wake Ofisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, George Ndata amesema bila kuwa na amani hakuna maendeleo wa siasa hivyo suala la amani limechukuliwa kuwa la kiraia na si vyombo vya ulinzi pekee.