NA ASHRACK MIRAJI, ROMBO,KILIMANJARO
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro,Nurdin Babu, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Godwin Chacha kutumia fedha za mapato ya ndani kukarabati madarasa chakavu katika Shule ya Msingi Kwaktau, lengo likiwa ni kuboresha mazingira rafiki kwa wanafunzi.
Ametoa maelekezo hayo Juni 13,2025 wakati wa ukaguzi wa madarasa mapya saba ya msingi na mawili ya elimu ya awali, matundu 16 ya vyoo, kichomea taka, jengo la utawala na uzio, vyote vikiwa na gharama ya Sh. Milioni 340.
Aidha,Babu amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, pamoja na timu yake kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya elimu yenye viwango bora na muonekano mzuri unaowavutia wanafunzi kuhudhuria shuleni kwa idadi kubwa.
Babu alisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote, hivyo ni muhimu kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma katika mazingira salama na yenye kuvutia.
Alieleza kuwa shule yenye miundombinu bora huwajenga wanafunzi kisaikolojia na kuwahamasisha kufikia malengo yao ya kielimu.
Katika ziara hiyo, baadhi ya wananchi wa eneo hilo walipata nafasi ya kueleza changamoto wanazokumbana nazo, hasa katika shule kongwe ambazo hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Babu aliwahakikishia kuwa Serikali iko makini na itaendelea kushirikiana na viongozi wa maeneo kuhakikisha kila mtoto anasoma katika mazingira bora.
Kwa upande wake, Chacha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo aliahidi kutekeleza maelekezo hayo kwa haraka kwa kutumia mapato ya ndani, huku akitoa wito kwa jamii kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya shule ili kudumisha ubora wake kwa vizazi vijavyo.