*YABAINISHA MALENGO YA MIAKA 50 IJAYO
*MOJAWAPO NI KUJENGA KIWANDA KIKUBWA CHA UCHAPAJI MIKOCHENI JIJINI DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesema katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimeimarisha uwezo wa kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali yahusuyo ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia ushahidi unaotokana na matokeo ya tafiti hizo.
TET imesema tafiti hizo zimekuwa zikifanywa na wao kwa ushirikiano na vyuo vingine vya ndani na nje ya Tanzania na kwamba zimesaidia pia kuimarisha mapato ya ndani ya taasisi hiyo.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo Juni 13,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba wakati wa semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea miaka 50 ya taasisi hiyo.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2020/21 TET ilishirikiana na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Agha Khan, Aga Khan Foundation (AKF) na EdTech Hub kufanya utafiti wenye lengo la kubainisha teknolojia ya TEHAMA iliyo nafuu, sahihi na endelevu itakayofaa kutumika katika kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini ili kuboresha matokeo ya wanafunzi katika ngazi ya elimu ya msingi kwa shule zilizopo vijijini.
“Utafiti huu ulitumia kiasi cha Sh. Milioni 850, tumepata matokeo ya utafiti huu na tunatarajia kuwa yatatusaidia kushauri teknolojia ambayo ni nafuu na inaweza kutumika katika mazingira ya vijijini,” amesema
Hata hivyo amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 TET imefanya utafiti na Chuo Kikuu cha Western Norway of Applied Sciences ambao unaojulikana kama ‘Kuona ni Kujifunza’ ambao lengo lake lilikuwa ni kubaini changamoto za uoni miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi na kutoa afua stahiki.
Amesema matokeo ya utafiti huo yamesababisha uhitaji wa kuandaa moduli kwa kutolea mafunzo kazini kwa walimu ili kuongeza umahiri wao katika kuwabaini, kuwachunguza na kutoa afua stahiki kwa wanafunzi wenye changamoto za uoni katika kujifunza kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na kwamba jumla ya fedha iliyotumika katika utafiti huu ni Sh. Milioni 950.
Amesema kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 TET inashirikiana na Vyuo Vikuu vya Georgetown, Delaware na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndaki ya Elimu kufanya utafiti unaojulikana kama “What Works Hub (WWH) for Global Education”.
“Kupitia utafiti huu kituo cha utafiti kiitwacho “TIE-Ed-Lab kimeanzisha. Kituo hiki kimejikita kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya ufundishaji na ujifunzaji kwa ujumla ili kuendelea kuimarisha utoaji wa maamuzi unaotumia na matokeo ya tafiti,” amesema
Amesema utafiti huo ni wa miaka mitano na utagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 7 na kuongeza kuwa katika miaka hiyo 50 wamefanikiwa kuongezeka kwa ushirikiano wa TET na taasisi nyingine za ndani na nje katika kutekeleza majukumu ya taasisi.
“Hadi mwaka 2025 TET imeingia makubaliano na Mashirika 35 kwa malengo mbalimbali kama matumizi ya akili mnemba (AI) katika ufundishaji na ujifunzaji, uandaaji wa maudhui ya kidijitali kwa ngazi mbalimbali,” amesema Dk. Komba
Akielezea malengo ya Taasisi hiyo Kwa miaka 50 ijayo,Dk.Komba amesema ni kujenga kiwanda kikubwa cha uchapaji
” TET ina malengo ya kujenga kiwanda kikubwa na cha kisasa cha uchapaji eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam, haya ni malengo ya miaka 50 ijayo “amesisitiza Dk.Komba.