NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam imemuhukumu kifungo cha miaka miwili jela au fauni ya Sh.1,000,000 Ofisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya Mpira wa Miguu ya ‘KENGOLD Sports Club’ Joseph Mkoko kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh.1,500,000.
Makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2024.
Awali ilidaiwa kuwa Ofisa huyo alipokea rushwa kutoka kwa mchezaji mmoja wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital’o ya Burundi, ili amsaidie kusajiliwa na ‘KENGOLD Sports Club’ na kupata upendeleo wa kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dk. Beda Nyaki Mei 30, 2025 na kufunguliwa Shauri la Jinai namba 13138/2025 huku upande wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa( Takukuru) ikisimamiwa na Mwendesha Mashtaka Imani Nitume.
Aliposomewa mashtaka yake, mshtakiwa alikubali na kesi iliahirishwa hadi leo Juni 11, 2025 kwa ajili ya kusoma maelezo ya awali ya kosa.
Leo, mshtakiwa alikumbushwa makosa yake na kuendelea kukubali na aliposomewa maelezo ya awali ya kosa pia alikubali, hivyo mahakama imemtia hatiani.