NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa kinara katika kuchangia gawio kwenye mfuko mkuu wa Serikali kwa taasisi za umma kwa mwaka 2025, ambapo imetoa gawio la Sh. Bilioni 181.1.
Gawio hilo limetolewa leo Juni 10,2025 Ikulu jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma.
Hata hivyo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekuwa mchangiaji wa pili kwa kuchangia fedha kwenye mfuko mkuu wa Serikali ambapo imetoa gawio la Sh.Bilioni 38.8 huku nafasi ya tatu imechukuliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kutoa gawio la Sh. Bilioni 29.8.
Taasisi zingine zilizotoa gawio kubwa mwaka huu chini ya taasisi zilizotajwa hapo juu ni pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) iliyotoa gawio la Sh. Bilioni 20.4 na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa gawio la Sh. Bilioni 19.2.
Wengine ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) iliyotoa gawio la shilingi bilioni 16.3 na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) iyotoa gawio la Sh.Bilioni 10.4.