NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali ina lengo la kuondoa Mashirika mizigo na kwamba haitavumilia baadhi ya mashirika hayo ya umma kuendelea kunufaika kwa kutumia rasilimali za umma bila kurejesha faida inayostahili kwa serikali.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 10,2025 katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi za umma, Rais Samia amesema kuwa zama zile za taasisi kuendelea kuchuma serikalini bila zenyewe kurudisha faida zimepitwa na wakati na hazipo tena.
Amesema kila shirika na taasisi zijitahidi kujibeba na kuibeba serikali na kwamba anataka mashirika yawe walinzi wa uwekezaji uliofanywa na serikali kwa kuboresha miundombinu na kupunguza upotevu ili kupata faida.
“Nimefarijika na hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kupunguza utegemezi wa Taasisi za Umma kutoka Serikalini ambapo nimejulishwa kuwa katika kipindi hiki, Taasisi za STAMICO (Shirika la Madini la Taifa) na TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) zimejitoa katika utegemezi wa ruzuku ya Serikali ya mishahara na uendeshaji na sasa zinakwenda kujitegemea,” amesema
Rais Samia amesema hiyo ni hatua kubwa na inayohitaji pongezi kwani fedha zile zilizokuwa zinatumika katika kuendesha mashirika hayo sasa zinakwenda kutumika katika miradi ya maendeleo na kwamba huo ni mwelekeo chanya na ni sehemu ya mageuzi aliyotarajia.
“Ni matumaini yangu kuwa huu ndiyo utakuwa mwelekeo kwa taasisi zingine kupunguza utegemezi serikalini na hatimaye kujitegemea kabisa. Wito wangu kwa taasisi nyingine mjitathmini. Kama wengine wameweza kujitegemea, na nyie mnaweza. Tuondokane na utegemezi na kuwa mzigo wa ruzuku ya Serikali,” amesema