NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za umma kuwa wabunifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 10, 2025 katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi za umma, Rais Samia amesema anafahamu kuwa taasisi zina changamoto mbalimbali lakini changamoto kubwa ni suala la upatikanaji wa mitaji.
Amesema serikali imetekeleza kwa kiasi fulani lakini bado mahitaji ni makubwa hivyo mageuzi ni pamoja na kuwa wabunifu, wasisubiri serikali itatue kila changamoto inayowakabili kama taasisi.
“Tutumie fursa mbalimbali zinazotuzunguka katika kutatua changamoto hizo ikiwemo soko la mitaji. Msajili wa Hazina nakuagiza ukafanye utafiti ili kuja na mapendekezo ya Taasisi zinazopendekezwa kujiorodhesha katika soko la hisa (ushiriki wa wananchi) katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
“Lengo ni kuwapa wananchi nafasi ya kumiliki mashirika haya na hatimaye kufikia maelekezo yangu ya mashirika ya umma kumilikiwa na wananchi badala ya kuwa mashirika ya Serikali. Kitendo hiki sio tu kitasaidia kupata mitaji bali pia kitawezesha wananchi kuwa wamiliki katika mashirika na rasilimali zao,” amesema
Hata hivyo Rais Samia amemtaka Waziri wa Mipango na Uwekezaji kuendelee kusimamia ukamilishaji wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma ili wasonge mbele na kwamba kama kuna changamoto zozote afahamishwe kwa lengo la kuhakikisha kuwa azma iliyokusudiwa kwa kuwa na Sheria ya Uwekezaji wa Umma ikiwemo suala la Mfuko wa Uwekezaji na kuwezesha usimamizi madhubuti wa Uwekezaji wa Serikali, linafikiwa.
“Ninakuagiza Msajili wa Hazina pamoja na vingozi wote wa Taasisi za Umma kuendelea kubuni na kusanifu mifumo ya TEHAMA mahsusi itakayoendelea kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yenu na hatimaye kusaidia utoaji huduma wa haraka na kuongeza faida kutokana na uwekezaji uliopo.
“Katika hili, pia niwatake viongozi wote kuhakikisha mifumo ya TEHAMA iliyopo inaendelea kuhuishwa ili iweze kuwa na mlingano mzuri wa taarifa na kuongeza tija kwa taasisi zetu,” amesema Rais Samia
Rais Samia amesema utekelezaji wa majukumu yoyote ya taasisi unategemea ubora wa rasilimali watu iliyopo na katika hilo, amemuagiza Msajili wa Hazina na Mamlaka nyingine husika kuendelea na jitihada za jumla za kuwajengea watumishi uwezo katika nyanja mbalimbali za kisasa pamoja na motisha stahiki ili kuongeza morali ya kazi na hatimae tija kwa taasisi.
Aidha amesema gawio alilolipokea leo ni kielelezo cha juhudi, uaminifu na uadilifu wa watumishi wa mashirika na taasisi hizo katika kusimamia rasilimali za umma.
“Taasisi zetu zinapaswa kuwa mfano wa ufanisi, uwajibikaji na tija. Hili, linawezekana iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kikamilifu,” amesema Rais Samia
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema kiwango cha gawio na michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma ambacho kinakabidhiwa kwa Rais Samia kimeongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh. Triloni 1.2 kutoka Sh. Bilioni 611 ambayo ilikusanywa mwaka jana.
Mchechu amesema “Rais nakumbuka mwaka jana Juni 11 tulipokutana hapa tulikukabidhi Sh. Bilioni 611 na hiki kilikuwa kiwango kilichukusanywa hadi kufikia tarehe ile kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma, ulipopokea gawio hilo ulituagiza kwamba mwaka unaofuata unataka kuona gawio limeongezeka na likiwa ni nono zaidi na Rais ili makamanda wako na watu wako na wasaidizi ujue wanatekeleza inabidi tufanye kazi hiyo kwa vitendo na tumetekeleza hayo”
“Mbele yako Rais ninayo furaha ya kukukabidhi gawio nono kuliko la mwaka jana na kwamba mpaka kufikia jana June 09, 2025 Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni moja (1) na Bilioni 28, kiwango hiki ni ongezeko la asilimia 68 kama tutalinganisha na ulichokuwa unakipokea mwaka jana na unachokipokea leo” amesema Mchechu
Mchechu amesema gawio hilo linajumuisha mashirika yote ya umma yaliyochini ya usimamizi wa ofisi ya hazina na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache na kwamba katika kiwango hicho kilichokusanywa mwaka huu ni mjumuisho wa gawio kutoka mashirika na kampuni zinazofanya biashara Sh. Bilioni 603.4 sawa na asilimia 59 ya makusanyo yote.
“Kiasi hicho kilichotolewa pia ni mjumuisho wa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi shilingi bilioni 363.4 na mapato mengineyo ni Sh.Bilioni 61 sawa na asilimia sita ya makusanyo yote,” amesema Mchechu
Amesema takwimu hizo ni ushahidi wa mwelekeo chanya na matokeo ya juhudi za mageuzi ya kiuendeshaji wanayotekeleza kwa maelekezo Rais Samia.
Hata hivyo amesema kiasi hicho kimekusanywa kutoka katika jumla ya taasisi na Mashirika 213 kati ya hayo ya umma ni 195 na 18 ni kampuni zenye hisa chache.
“Hii inamaanisha kuwa mashirika 57 hayajatoa gawio bado ambayo ni asilimia 22 ya mashirika yote,” amesema
Aidha Mchechu amesema pamoja na mafanikio yote hayo bado wana kazi kubwa ya kuendelea kufanya maboresho ya kiutendaji na kiuendeshaji ikiwamo kuhakikisha idadi ya mashirika yanayochangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali inaongezeka, utegemezi wa ruzuku ya Serikali katika uendeshaji unapungua na mashirika yanayojiendesha kwa hasara yanaondoka katika kundi hilo.
“Kwa niaba ya viongozi wa taasisi za umma waliopo hapa, naomba kukuahidi kuwa tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na kuulinda uwekezaji wa umma kwa wivu mkubwa. Aidha, naomba kutoa shukrani za dhati kwa uongozi wako madhubuti na kwa kutuhimiza kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu,” amesema
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliahidi kuendelea kuhakisha wizara yake inasimamia kikamilifu maono ya Rais ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kutoa matokeo bora kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha 2025/2026, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imejipanga kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha usimamizi na tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.
“Lengo letu ni kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi hizi zinaendelea kutoa matokeo bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” amesema Prof. Mkumbo