NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Godfrey Nyaisa amewataka Watumishi wa Wakala hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ili kulinda na kuinua taswira ya Taasisi kiutendaji kwa kuendelea kutumia ubunifu kwenye kazi.
Nyaisa ameyasema hayo leo Jumanne Juni 10, 2025 alipokuwa akizungumza na watumishi wa BRELA walipompokea wakati akitoka kwenye hafla ya utoaji gawio na michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma ambapo BRELA ilitoa gawio la Shilingi Bilioni 20.4 na kutunukiwa Tuzo katika kipengele cha Taasisi iliyofanya vizuri kwenye utoaji gawio kwa wakati kwa mwaka 2025.
Aidha, Nyaisa amewasisitiza watumishi kuendeleza juhudi katika kazi na kuwa wabunifu kwa lengo la kuhakikisha mapato hayo hayashuki ili kutimiza malengo ambayo taasisi imejiwekea katika kuchangia maendeleo ya nchi.
“Kwa hiki kilichofanyika leo, mmemsikia Mhe. Rais Dk.Samia Suluhu Hassan akipongeza Taaasisi zilizofanya vizuri na mimi natamani tusitake mapato haya yashuke, tumekuwa tukipanda. Mwaka jana tulitoa bilioni 18.9 na mwaka huu bilioni 20.4 na tunategemea tutapanda kufikia bilioni 21,’’ amesema Nyaisa.
Amesema tuzo hiyo ni matunda ya kazi iliyofanywa kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 01 mwaka 2024 hadi sasa na baada ya upembuzi kufanyika BRELA imeonekana kufanya vizuri hivyo amewaomba watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuonekana kwenye maeneo mbalimbali kama vile kwenye maonyesho ambayo wanashiriki.
BRELA ni miongoni mwa Taasisi zaidi ya 300 zinazotoa gawio kwa Serikali ambapo kwa wastani imetoa shilingi bilioni 16.8 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.