NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIBU Mwenezi Taifa wa Chama cha NCCR Mageuzi, Elisante Ngoma ametangaza rasmi kujiunga na ACT Wazalendo huku akikishukuru chama chake cha awali kwa heshima kubwa aliyopata ya kushika nafasi mbalimbali nyeti.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutangaza uamuzi huo, Ngoma amesema amejiunga na ACT – Wazalendo Mara baada ya kuona chama cha NCCR Mageuzi kimepoteza dira ya kupambana na CCM.
Amesema wakati umefika sasa wa kuachana na siasa za kuwalaghai watanzania, siasa zisizoangalia maslahi ya wananchi bali maslahi ya wachache na kwamba amejiunga na ACT Wazalendo ili aunge mkono juhudi za chama hicho zinazotanguliza utu, uwajibikaji na
maendeleo ya kweli ya kila Mtanzania.
“Nimevutiwa na jitihada za ACT Wazalendo kuwalea vijana kiuongozi na kuwapa jukwaa kuonesha uwezo wao. Nimechoshwa na siasa za kufifisha jitihada za vijana kukua kisiasa kwa kuwawekea vikwazo na kuzima sauti zao. Ninakuja ACT Wazalendo kama kijana ambaye nipo tayari kupambana kwa nguvu zote
kutekeleza malengo ya chama.
“Nimevutiwa na mipango ya ACT Wazalendo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 kupitia kauli mbiu ya ‘Tutashiri tukipambana, tutapambana tukishiriki’. Uzoefu wa kisiasa umetuonesha hivi sasa nchini hakuna Tume Huru ya Uchaguzi. Hata hivyo, dira ya ACT Wazalendo kushiriki kwenye uchaguzi kama jukwaa la kimapambano ni uamuzi sahihi,” amesema
Aidha amesema ili kuonesha uzito wa hoja yake atakisaidia chama chake kutekeleza malengo yake nyumbani Same Magharibi na maeneo mengine nchini.
“Ninajiunga na ACT Wazalendo kutoa mchango wangu katika kuiondosha CCM madarakani. Utawala wa CCM hausikii tena sauti za watu, haujali tena mateso ya
wanyonge, utawala uliojaa kiburi na maamuzi yasiyo na mashiko. Utawala unapofikia hapo hupoteza uhalali wa maadili, hata kama una nguvu kimfumo,” amesema