NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WASANII wa muziki nchini wametakiwa kusajili kazi zao na kuzilinda kupitia mifumo rasmi ya miliki bunifu ili kunufaika kiuchumi na kulinda kazi zao dhidi ya wizi wa ubunifu.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo Mei 21, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, katika maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu Duniani kwa mwaka 2025.
Nyaisa amesema licha ya muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya nchi, wasanii wengi bado hawajachukua hatua ya kusajili kazi zao, jambo linalowanyima fursa ya kunufaika na kazi hizo kisheria.
“Tunasisitiza muziki si burudani tu, ni biashara. Na biashara yoyote inalindwa. Wasanii wengi wanapoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” amesema.
Kauli mbiu ya mwaka huu kimataifa ni “Muziki na Miliki Bunifu Tanzania: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.”
Nyaisa amesema BRELA imekuwa ikitoa elimu kwa wasanii kuhusu haki zao za ubunifu na kuwasogezea huduma ili waelewe namna bora ya kulinda kazi zao.
“Wapo wasanii wa zamani ambao nyimbo zao bado zinapigwa hadi leo lakini hawapati chochote kwa sababu hawakuzisajili. Hili ni pigo kwao na kwa familia zao,” amesema.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia yamekuwa na pande mbili; yamefungua fursa kwa wasanii lakini pia yameongeza changamoto ya matumizi holela ya kazi za muziki bila ridhaa ya wasanii.
BRELA imesema itaendelea kushirikiana na taasisi kama COSOTA ili kuhakikisha kazi za ubunifu zinalindwa na zinakuwa chanzo thabiti cha kipato.
Katika tukio hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo, alikuwa mgeni rasmi. Alipongeza hatua ya kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Miliki Bunifu, akiitaja kuwa dira muhimu ya kuendeleza ubunifu nchini.