NA ASHRACK MIRAJI,SAME,KILIMANJARO
MKUU wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amepiga marufuku mara moja utiririshaji wa maji machafu yenye kemikali kutoka katika Kiwanda cha kuchakata mkonge kinachomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MELT), kilichopo katika shamba la mkonge la Hassan Sisal Estate, Kata ya Makanya.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia wasiwasi wa uchafuzi wa mazingira na athari za kiafya kwa wakazi wa Makanya na maeneo jirani yanayopata huduma ya maji kupitia mto unaopita karibu na kiwanda hicho.
Mgeni alitembelea baadhi ya maeneo ya mto huo na kujionea hali ya maji yaliyobadilika rangi kuwa nyeusi na kutoa harufu kali, hali iliyomsukuma kufika kiwandani kujiridhisha na chanzo cha uchafuzi huo.
“Kuanzia sasa ni marufuku kuelekeza maji machafu yenye kemikali kwenye mto ambao maji yake yanatumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu, hususan kilimo na mifugo. Baadhi ya wananchi wanayatumia moja kwa moja,” amesema DC Mgeni
Amesisitiza kuwa uamuzi huo unalenga kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.
Aidha, Mgeni alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha wataalam wa mazingira na afya wanafika kiwandani hapo kufanya uchunguzi wa kina ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
“Serikali inathamini uwekezaji, lakini ni lazima wawekezaji wazingatie sheria na taratibu ili kulinda afya za wananchi na kukuza uchumi wa taifa kwa njia endelevu,” amesema.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kutoridhishwa na hali ya usafi kiwandani hapo na kuwataka wasimamizi wa kiwanda kufanya usafi wa maeneo yao ya kazi ili kuepuka hatari ya magonjwa ya mlipuko kwa wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 129 kinakataza mtu yeyote kuachilia maji taka au taka hatarishi moja kwa moja kwenye mazingira bila kibali au bila kuyatibu.
Sheria hiyo pia inataka viwanda kuwa na mitambo ya kisasa ya kutibu majitaka kabla ya kuyamwaga kwenye mazingira. Endapo ukiukwaji utabainika, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) itachukua hatua kali dhidi ya wahusika.