NA MWANDISHI WETU,DODOMA
VYAMA 18 vya siasa vyenye usajili kamili, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wamesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 leo Jumamosi Aprili 12, 2025 jijini Dodoma.
Vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform (NCCR), Union for Multiparty Democracy (UMD), National League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA).
Vyama vingine ni Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).
Kwa upande wa Serikali Kanuni hizo za maadili zilisainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi na kwa upande wa Tume alisaini Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele.
Awali akizungumza kabla ya utiaji saini, Jaji. Mwambegele alivishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano wao wakati wote wa uandaaji wa kanuni hizo za maadili.
“Tunawashukuru viongozi wote wa Vyama vya Siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano Tume katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali hususan yale yanayohusu mchakato wa maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo uandaaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambazo tupo hapa leo kwa ajili ya kutia saini kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema Tume imeandaa kanuni hizo za maadili ambazo zitatambulika kama Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024.
“Baada ya kukamilisha maandalizi ya rasimu ya Kanuni hizo, Tume iliziwasilisha kwenu (vyama vya siasa na Serikali) kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yenu kuanzia tarehe 1 Machi, 2025 hadi tarehe 14 Machi, 2025.
“Maoni yenu yamejumuishwa katika Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 tutakazotia saini hii leo.
” Napenda kutoa shukrani za dhati kwenu kwa ushiriki wenu katika kuandaa rasimu hiyo kwa kutoa maoni yenu na kuyawasilisha Tume kwa wakati,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha rasimu ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, Tume iliwarejeshea tena wahusika Rasimu ya Kanuni hizo Aprili 4, 2025 na kuwaalika kwa ajili ya utiaji saini leo Aprili 12, 2025 na kwamba hakuna maoni tofauti yaliyotolewa.
Wakati huo huo ,Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Kailima, R. K wakati akifafanua mambo muhimu yaliyomo kwenye kanuni hizo amesema vyama vya siasa vina wajibu wa kufanya kampeni za kistaarabu na kujiepusha na mambo yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani.
Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake ina wajibu wa kutoa fursa sawa ya vyama vya siasa kufanya kampeni, kutumia vyombo vya habari vya umma na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na hali ya utulivu na amani.
Kwa upande wa Tume, Kailima amesema inawajibika kwenye mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na wa haki na kuhakikisha kunakuwa na usawa katika mchakato wa uchaguzi.
Amesisitiza kuwa chama ambacho hakijasaini maadili hayo hakitopata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo nyingine zote zitakazofanyika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.