NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu inayotarajiwa kufanyika Aprili 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu orodha ya walioteuliwa kuwania tuzo hiyo.
Mkenda amesema lengo la tuzo hiyo ni kuhifadhi historia, kukuza uandishi bunifu na utamaduni wa watu kupenda kujisomea kitabu mara kwa mara.
Amesema kuwa serikali inataka kuhamasisha utamaduni wa kusoma vitabu nchini ndio maana wameileta tuzo hiyo kwa lengo la kuhamasisha watu waweze kutenga muda wa kujisomea vitabu.
“Watanzania wengi hawana utaratibu wa kujisomea vitabu, hivyo tunaamini kwa kutumia waandishi wetu nchini wataweza kuandika vitabu na kuhamasisha watu kusoma vitabu”. amesema Prof. Mkenda.
Amesema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mwandishi mzuri aliweza kuandika vitabu mbalimbali na namna amechangia kukuza lugha ya kiswahili hivyo kumuenzi kwake wameamua siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake kuwepo kwa utoaji wa tuzo hizo.
“Tukio hili la tuzo ni kubwa na linatokea siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere ambaye si tu alikuwa Rais wa Tanzania na mwanasiasa maarufu duniani bali alikuwa mwandishi bunifu katika maishairi na kazi za kisaiasa, aliandika vitabu pia,” amesema Profesa Mkenda
Naye Mwenyekiti wa Kamati wa tuzo hiyo, Profesa Penina Mlama amesema washiriki hao walioteuliwa, 10 watawania tuzo ya uandishi wa vitabu vya riwaya, 10 vitabu vya tamthiliya, 10 vitabu vya ushairi na wengine saba vitabu vya hadithi za watoto.
Amesema tuzo ya riwaya na waandishi wake kwenye mabano ni zawadi ya simu janja ( Dk Abbas Amal), Taifa jipya (Ahmed Mwaita), Damu nzito (George Lauwo), Mashahidi kutoka kuzimu (Ibrahim Mkamba), Bweni la wavulana (Lucas Lubango), Kuokoka (Majaliwa Sued), Jeneza la taifa (Maundu Mwingizi), Udi na Uvumba (Philip Oyaro), Mlezi wa Vizazi (Richard Mziray) na Kilicho Chetu ( Zakaria Riwa).
Kwa upande wa ushairi, amesema wanaoshindanishwa ni Adili Mwinyiae (Yunge), Ally Mchanyato (Tuzo ya usomaji), Ally Isuka (Nikifa Msinizike), Bakari Makame (diwani ya tafakuri), Hussein Abdallah (Diwani ya Urathi wa Mjumu), Kombo Omar (Kisima cha Giningi), Mbaruku Mohammed (Utenzi wa Nana Mkombozi), Peter Komba (Mashairi ya Maisha), Said Ramadhan (Pendo la mama kiboko) na Sharifa Mussa (Pambazuko).
“Wanaowania tuzo hiyo kwa upande wa hadithi za watoto ni Corona Cermak (Tembo zimamoto), Hafidhi Makame (Siafu na Majimoto), Lilian Mbaga (Hatima yangu),
Mwanacha Omary (Mwisho wa zarau),
Paulina Lugabulila (Dieisha la Ajabu),
Shifaa Feisal (Maua na Mji wa Maweni),
Tune Salim (Maziwa ya Kuku).
“Kwa upande wa tamthiliya ni Ally Ngagesa (Kijarida), Bupe Kagute (Anne na Annelisa), David Shaba (Beti ya Mauti),Elithabeth Mahenge (Pambana), Faraji Manoni (Kovu la Maisha), Ignas Mkindi (Mwale wa Matumaini), Murungi Katabarula (Zaidi ya Majirani), Said Kileo (Mwangaza ) Sajida Athumani (Mwangaza wa Mvita) ma Tyatawelu Kingu (Alama ya Kuzaliwa),” Amesema Profesa Mlama
Aidha amesema mshindi wa kwanza atapata zawadi ya Sh. Milioni 10, ngapi, cheti na muswada wake kutachapishwa na serikali na kisha kusambazwa shuleni na maktaba za taifa huku mshindi wa pili atapata Milioni Saba na cheti na mshindi wa tatu ataondoka na milioni tano na cheti.
Naye Mkurugenzi Mkuu TET, Aneth Komba amesisitiza kuwa mshindi wa kwanza katika tuzo hiyo atajipatia kiasi cha Sh. Milioni 10 /-na vitabu vyake kuchapishwa na serikali na kusambazwa katika shule zote za serikali nchini kwa uwiano wa shule moja vitabu 14.
Amesema kupitia tuzo hiyo yenye lengo la kukuza sekta ya uchapishaji wameweza kuchangia kuikuza sekta hiyo kwani kila mwaka wanakuwa na mzabuni mmoja wa uchapishaji ambaye ndio uchapisha vitabu kwa mwaka wa fedha.