NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti hizo za mwaka 2023/24 zimekabidhiwa kwake na CAG, Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu Takukuru, Crispin Chalamila leo Alhamisi Machi 27, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya viongozi wakuu wa nchi.
Amesema ni matumaini yake kuwa taasisi hizo mbili zitaendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na uzalendo wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa na wao serikali wapo tayari kufanyia kazi yale yote yaliyopendekezwa na kuelezwa katika ripoti hiyo ili kuweza kujenga utawala bora ndani ya nchi.
“Sisi upade wa Serikali tuko tayari kuendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizi mbili, tutasikiliza vizuri, tutafuatilia vizuri mjadala wa Bunge kwenye taarifa ya CAG na Takukuru. Tutakwenda kufanyia kazi vizuri yale yote ambayo yameelezwa ili hatimaye tuweze kujenga utawala bora ndani ya nchi yetu,” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia anayasema hayo wakati ripoti hizo zina mapendekezo ya namna ya kufanya ili kuongeza ufanisi katika mashirika, mapato ya Serikali na utumishi wa umma baada ya kurekodi hasara, ubadhirifu pamoja ukwepaji kodi katika mwaka wa fedha wa 2023/24.