*Ni kupitia mazungumzo kati ya Dk. Biteko na Waziri wa Petroli na Gesi
Asilia India
*Gesi, Nishati Safi ya Kupikia na Bayofueli zatajwa
*India yaipongeza Tanzania usambazaji umeme vijijini
*Dk. Biteko akaribisha wawekezaji,wafanyabiashara kutoka India
NA MWANDISHI WETU, NEW DELHI,INDIA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa
India, Hardeep Singh kuhusu nia ya nchi hiyo kuzidi kuimarisha
biashara kati yake na Tanzania kupitia sekta binafsi, kufanya
uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati na kujengea uwezo wataalam.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini New Delhi nchini India katika
Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati nchini humo.
Dk. Biteko amemweleza Waziri Singh kuwa milango ya uwekezaji
Tanzania ipo wazi na kampuni mbalimbali kutoka India zinaweza
kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya umeme, usambazaji wa
gesi ya mitungi (LPG) na uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Bulk
procurement) kwani kunahitajika washindani wengi ambao watatoa uhakika
wa uwepo wa mafuta wakati wote.
“ Tanzania tumejikita katika kuhakikisha tunatumia kila rasilimali
tuliyonayo ili kuwa na nishati ya kutosha ikiwemo umeme ili kukidhi
mahitaji ya wananchi,” amesema Dk.Biteko.
Aidha, ameeleza kuhusu umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika
kuendeleza miradi mbalimbali akitolea mfano kuwa, ili Tanzania
ijitosheleza kwa mahitaji ya nishati inahitaji Dola za Marekani
Bilioni 12 ambazo kupatikana kwake lazima sekta binafsi ihusishwe
hivyo kupitia kwa Waziri Singh, amekaribisha wawekezaji kutoka India
kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati nchini.
Kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Nishati India amesema kuwa
Tanzania imefaidika na ushiriki wake katika Wiki hiyo kwani India
tayari imeshapiga hatua kwenye Sekta ya Nishati hivyo imekuwa ni
sehemu maalumu ya kujifunza zaidi kuhusu sekta, kubadilishana uzoefu na
kunadi fursa za uwekezaji ikiwemo duru ya tano ya uendelezaji wa
visima vya mafuta na gesi asilia Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe.
Hardeep Singh amesema kuwa India ina uhusiano mzuri wa kibiashara na
Tanzania ambapo biashara kati ya pande hizo mbili imezidi kuimarika na
kueleza kuwa nchi hiyo imejipanga kuimarisha zaidi biashara yake kwa
Tanzania.
Ameeleza kuwa, nchi hiyo pia kupitia Sekta binafsi inataka kuwekeza
kwenye usambazaji wa mitungi ya gesi nchini hasa katika kipindi hiki
ambacho Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati
Safi ya Kupikia huku akieleza kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kwa
kusambaza mitungi ya gesi kwa asilimia 99.9 kwa wananchi wake.
Ameongeza kuwa India imeamua kuwekeza kwenye uendelezaji wa Mafuta na
Gesi Asilia ambapo baadhi ya kampuni zake zimejitokeza kushiriki Duru
la Tano la kunadi vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia linalotarajiwa
kufanyika mwaka huu mwezi Machi nchini.
“ India pia tupo tayari kuwekeza kwenye gesi ya kusindika (LNG),
bayofueli pamoja na kushirikiana na Tanzania katika masuala ya
kitaalam yanayohusu Sekta ya Nishati kwa kuwajengea uwezo zaidi
wataalam wa Tanzania na pia kuwa na programu ya kubadilishana wataalam
kati ya Tanzania na India,” amesema Singh
Pia, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kwenye usambazaji wa
umeme hususan vijijini na kwa jinsi inavyotekeleza mkakati wa nishati
safi ya kupikia kwa namna mbalimbali ikiwemo kuweka ruzuku kwenye
mitungi ya gesi.
Vilevile, Waziri Singh amempongeza pia Dkt. Biteko kwa hekima zake na
ukomavu ambao anauonesha pale anapoieleza dunia kuhusu masuala ya
uendelezaji wa rasilimali zinazoweza kuzalisha umeme ambazo Bara la
Afrika imebarikiwa nazo lakini mpaka sasa hazijaendelezwa ipasavyo
kutokana na misimamo ya kidunia ikiwemo makaa ya mawe ambayo
yakiendelezwa yatazidi kutoa uhakika wa uwepo wa nishati ya kutosha.
Mazungumzo kati ya viongozi hao yamehudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye anamwakilisha
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Idd Kassim, Kamishna wa Umeme na
Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Andilile.