NA JANETH
JOVIN,DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kusaidia mipango yote ya Kidemokrasia yenye lengo la kukomesha mapigano na machafuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Februari 8,2025 Ikulu Jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha viongozi na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) waliokutana kwa lengo la kujadili na kuangalia hali ya usalama nchini Congo.
Amesema Congo ambayo ipo SADC bado inaendelea kukabiliwa na migogoro na machafuko ambayo yanaleta madhara makubwa kwa maisha ya binadamu na kuathiri biashara pamoja na uchumi mipakani.
“Kutokana na hicho kinachoendelea Congo, nchi zetu za SADC na EAC zinawajibu kushughulia suala hili la amani ambalo lina athiri, tumekutana leo kwa lengo la kutafuta suluhisho la kudumu ambalo ni jumuishi ili wananchi wa DRC wafurahie amani ambayo wameisubiri kwa miaka mingi.
“Nchi yangu itaendelea kusaidia mipango yote ya Kidemokrasia ili kukomesha mapigano huko Congo, kuwepo kwetu Dar es Salaam kunatoa fursa ya kuweza kujadiliana ni kwa namna gani tunaweza kukomesha vita na kupunguza madhara zaidi kwa binadamu,” amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia amesema kuwa ombi lake kwa Wakuu hao wa nchi ni kutafuta jitihada za kukomesha machafuko na kuleta amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Naye Rais wa Kenya na mwenyekiti wa EAC, William Ruto amesema jitihada zilizofanywa na Jumuiya hizo mbili ni kukutana kwa pamoja katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa Congo uliosababisha vifo vya watu, kwa njia ya kidiplomasia.
Amesema kukubaliana kwao ni sasa katika kuchukua hatua na kuwaonea huruma mamilioni ya watu ambao wapo katika hatari ya kupoteza maisha na maendeleo yao ya Kiuchumi.
“Tumeona mamilioni ya watu wakihama makazi yao, mgogoro huo unaonesha athari kwa nchi nyingi hivyo tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia DRC kwa kuwapatia misaada. Mgogoro wa Congo ni tete na unahusisha pande mbalimbali na umedumu muda marefu, tusitumie mabomu katika kupata suluhu tuangalie suluhu jumuishi kwa kuangalia chanzo,” amesema Ruto
Ruto amesema mazungumzo ya amani siyo udhaifu ni busara ya pamoja na yanaonesha usikivu wakiwa na lengo la pamoja la kupata matokeo mazuri na sio vita na kwamba kuelekea kusuluhisha mgogoro huo inahitajika uungwaji mkono kisiasa
=”200″ class=”alignnone size-medium wp-image-15224″ />
Kwa upande wa Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC, Emmerson Mnangagwa amesema mkutano huo ni ushahidi wa dhamira yao ya pamoja na kwamba juhudi hizo zinawawezesha kuchukua hatua za haraka ili kusitisha vita katika nchi zao.
Amesema hali tete inayoendelea, migogoro iliyopo na ongezeko kubwa la wahamaji lina madhara makubwa si tu Congo bali katika nchi zingine za EAC na SADC.
“Tunatakiwa kuendelea kushikimana kama tulivyokuwa tunapambana kutafuta uhuru dhidi ya wakoloni, tutumie fursa hii kuwa na suluhisho la pamoja ambalo lina lengo la kukomesha vita na kuleta amani ya kudumu Congo.
“Maslahi ya wananchi wa Congo yanapaswa kuwa mbele katika mipango hii tutakayoifanya, mkutano huu unatakiwa kutuwezesha kupiga hatua za haraka zitakazosaidia kusoga mbele,” amesema Rais Mnangagwa.