NA ATUPAKISYE MWAISAKA, DAR ES SALAAM
OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa amewataka Watumishi wa Taasisi hiyo kuzingatia maadili na kuweka nidhamu katika utendaji kazi ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Nyaisa ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu na watumishi wote wa BRELA kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dar es Salaam kwa lengo la kukumbushana majukumu, kusikiliza changamoto za kiutendaji na kuzitatua pamoja na kuwapongeza wafanyakazi bora na kuwaaga watumishi waliostaafu.
“Napenda kuwasisitiza sana suala la nidhamu ya kazi, tujenge utamaduni wa kuheshimu nafasi tulizonazo na tuwe waadilifu mahala pa kazi ili hata ukienda taasisi nyingine nje ya BRELA waone kweli umejifunza kazi na unaiweza kufanya kwa ufanisi” amesema Nyaisa
Ameongeza kuwa,kila mmoja atambue wajibu wake na kuutekeleza, na kuwataka wafanyakazi hao watambue kwamba juhudi za mfanyakazi mmoja mmoja ndizo zinazompa nafasi Ofisa Mtendaji Mkuu kuonekana kuwa anafanya kazi na kuipa sifa Taasisi kwa ujumla.
Aidha Nyaisa amesema, ataendelea kufanyia maboresho ya kiutendaji changamoto zilizopo na kuwataka wafanyakazi kuendelea kuwa wavumilivu wakati misingi ya maboresho ikiendelea kuwekwa kwa ajili ya watumishi wote.
Kikao hicho kilifuatiwa na hafla ya kuwapongeza wafanyakazi bora na hodari waliofanya vizuri kwa mwaka 2023/2024 ambao walitunukiwa vyeti na zawadi kwa wafanyakazi bora huku mfanyakazi Hodari wa Taasisi akipata cheti na Sh.Milioni tatu.
Watumishi bora waliopata zawadi na cheti ni Vicente Nyanje, Abdulkarim Nzori, Boniface Ngugi, Abas Cothema, Gwamaka Mwankenja, Mwajabu Goma, Swedi Jabiri na Onesmo Mushi ambaye pia amekuwa mtumishi Hodari wa mwaka na kuondoka na Sh.Milioni tatu za Kitanzania.
Katika kikao hicho pia watumishi waliostaafu waliagwa na kupongezwa kwa mchango wao walioutoa kwa taasisi, ambapo kwa kutambua hilo Ofisa Mtendaji Mkuu Nyaisa alitoa zawadi maalumu ya vocha yenye thamani ya Sh. Milioni moja kwa kila mtumishi ambayo watakwenda kufanya manunuzi ya kitu chochote.
Wafanyakazi hao waliostaafu utumishi wao kwa mujibu wa sheria ni pamoja na Deo Meela, Andrew Mkapa, Gloria Binamungu Gloria Mbilimonywa
Sambamba na hayo Nyaisa aliwapongeza pia watumishi ambao wamekuwa wakiandika makala maalumu za kitaalam kuhusu majukumu yanayofanywa na BRELA kwa lengo la kutoa elimu kwa umma na kutoa rai kwa watumishi wingine kufanya hivyo ili umma uweze kujua shughuli mbalimbali za kiutendaji na hivyo wafanyabiashara kuweza kurasimisha biashara zao.
Watumishi waliotambuliwa mchango wao ni pamoja na Stanslaus Kigosi, Isdor Nkindi, Menrad Rweymamu, Abdul Songoro, Sweetness Madata, Calvin Rwambogo, Andrew Mares na Tawi Kilumile.