NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema hadi kufikia mwaka 2030 watanzania wote watakuwa tayari wamefikiwa na umeme kutokana na mipango madhubuti iliyopangwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Serikali unaoendelea katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).
Amesema kutoka na kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kufanikiwa hivyo suala la umeme pia litafanikiwa kwa kila mtanzania.
Amesema hadi kufikia mwaka 2030 Serikali ya Tanzania imekusudia kuhakikisha zaidi ya asilimia 75 ya watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia.
Mramba amesema mkutano huu kufanyika hapa ni kama namna nyingine kutambua kazi kubwa ambayo nchi ya Tanzania imeweza kufanya.”Ni uongozi wa Rais Samia katika nishati ya kupikia ambapo Rais Samia ametambulika Duniani kama ni Champion katika eneo hili la nishati ya kupikia na Tanzania tupo mstari wa mbele katika utekelezaji wa jambo hili.
”Ambapo sisi tumeonekana kuwa miongoni mwa nchi chache tumeonyesha mfano ambapo Tanzania tayari imetengeneza mkakati wa utekelezaji wa nishati safi ya kupikia ambapo mkakati unaotoa miaka hadi 2034 kuweza kuwaamisha watanzania wote kutoka katika nishati isiyokuwa safi na kutumia nishati safi,”amesema
Aidha amesema pia suala la Tanzania kuondokana na mgao wa umeme hili ni suala lingine ambalo Tanzania limetoa ujumbe kwa mataifa mengi ya Afrika juu ya uwezo na dhamira ya serikali ya Tanzania ya kuweza kuwafikishia wananchi wake umeme wa uhakika na kuondokana na matatizo ya changamoto nyingi za umeme.
”Mkutano huu unatuhakikishia mwaka 2030 Watanzania asilimia 100 wataweza kufikiwa na miundombinu ya umeme na wataweza kupata umeme na katika kipindi hicho watanzania ambao umeme umeingia katika nyumba zao wasiwe chini ya asilimia 75,pia katika kipindi hicho tunataka chini ya asilimia 75 wawe tayari wamepata nishati safi ya kupikia,” amesema
Amesema mkutano huu utawaachia watanzania wakiwa wametengeneza mahusiano makubwa na wadau mbalimbali sekta binafsi,washirika maendeleo,mabenki pamoja na watafiti.
Mramba amesema katika mpango huu serikali ya Tanzania imekusudia kuunganisha mita mpya milioni8.5 katika miaka mitano ijayo.