NA MAGENDELA HAMISI,DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Manispaa ya Ubungo Elias Ntiruhungwa amechangia Shilingi 1,000,000 kwa taasisi ya Sambaza Upendo ambayo iko chini ya Dk. Askofu Leonard Ntibanyiha wakati wa tafrija ya kugawa misaada ambayo imefanyika katika Kanisa la Goran, Mbezi Luis jijini Dar es Salaam.
Mchango huo umetolewa jana Septemba 21, 2024 na Ofisa Mazingira wa Manispaa hiyo, Nice Vahaye aliyefika katika shughuli ya kutoa misaada kwa wakazi wa Mtaa wa Matope, Mbezi Luis, wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo wajane, wazee na yatima akimwakilisha Mkurugenzi huyo.
“Nimekuja hapa kumwakilisha Mkurugenzi wetu, kwa hakika tumeona juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Sambaza Upendo na kutokana na changamoto ambazo wamezisema hapa ikiwemo ukosesefu wa eneo la kujenga Kituo na Shule, ukosefu wa gari na nyingine, yote kwa pamoja ni fedha, hivyo natoa Sh.Mil 1.
“Pia tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha juhudi hizo zinaendelea kuhimalika kwa maslahi ya watanzania wote hususani kwa wanaoishi katika mazingira magumu na kwa kufanya hivi tutawaondelea mawazo maovu na amani itadumu milele na hiyo ndio nguzo yetu,” amesema.
Pia Mchungaji Aman Kayuni, wa Taasisi ya Sambaza Upendo ametanabaisha kwamba lengo la kusambaza upendo ni kuingiza matendo kwa kubeba agizo la Mungu, linalosema “Nendeni mkayafanye mataifa yote yakawe wananafunzi”.
“Pia Yesu anasema, mkihudumia hawa mmenihudumia mimi” na kwa namna hiyo kwa jina la Yesu ambalo ndio msingi na upendo wa msalaba uliosababisha akafa msalabani kwa namna moja au nyingne inatulazimu sisi Sambaza Upendo, kuwakusanya watu kila tunapojaaliwa kuweza kuwahudumia, kwa neno, kwa chakula na mahitaji mengine kwa namna tunavyoweza kushauriana”, amesema.
Akizungumzia masuala yanayojiri sasa ya utekaji, mauaji, amesema Yeu alitumia neno kuponya mioyo ya watu, hivyo moyo ya watu usipopata neno ni ngumu kutengenezeka kibinadamu, kinachotakiwa kwa jamii ni kuvua utu wao wa zamani na kuvaa mpya hivyo ndivyo Mungu atakavyoondoa hali ya mauji, uvivu .
“Ombi letu kwa jamii, wanatakiwa wajikite zaidi katika neno la Mungu ili kuondoa roho ya utekaji, mauji, ubakaji, neno la Mungu likiingia katika mioyo ya watu biblia inasema, neno ni moto inayoyayusha roho ovu na hazitaweza kuwepo”, amesema.
Naye Mwenyekiti wa Wajane, Wilaya ya Ubungo, Josephine Eliazari, amesema wanayofuraha kujumuishwa pamoja na kupatiwa misaada mbalimbali na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kufanya hivyo na si kuwaachia jukumu hilo, taasisi ya Sambaza Upendo.
Taasisi hiyo, jana iliendelea na mchakato wake wa kugawa misaada ya nguo katika viunga vya Mbezi Luis, kwa wasiojiweza wakiwemo watoto yatima, wajane, wazee na makundi mengine yasiyojiweza kama ambavyo imekuwa ikifanya katika maeneo mengine tangu mwaka 2021, jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.