NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ILI kuhakikisha kero mbalimbali zinazoukabili mtandao wa barabara zinapatiwa ufumbuzi sahihi,Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeeleza mafanikio yake kwa miaka saba tangu ilipoanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini Julai Mosi, mwaka 2017.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara zote nchini.
Lengo kuu la matengenezo ya miundombinu ya barabara ni kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika katika maeneo mbalimbali Tanzania nzima.
Aidha kwenye suala la kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za wilaya lengo lake ni kuzifanya ziweze kupitika katika misimu yote ya mvua.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff alipokuwa akieleza mafanikio ya taaaisi hiyo katika Kikao Kazi cha Wahariri na Waandishi wa Habari Septemba 2,2024 jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) kama ulivyo utaratibu wao wa kuwakutanisha Wanahabari na Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kuzungumza nao.


Mhandisi Seff amesema TARURA itaendelea na matengenezo hata pale madaraja na barabara vitapokamilika ili miundombinu hiyo kudumu kwa muda mrefu.
Sambamba na hilo ni kuzipandisha hadhi barabara kutoka udongo kuwa changarawe, kutoka changarawe au udongo na kuwa barabara za lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kijamii na kiuchumi
Aidha Mhandisi Seff ameeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yao wanatumia teknolojia mbadala pamoja na malighafi za ujenzi zinazopatikana maeneo ya kazi ikiwemo mawe.
Amedadavua kuwa lengo la kutumia malighafi na teknolojia katika ujenzi na matengenezo ya barabara ni kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira.
“Serikali ina dhamira ya kuboresha na kujenga barabara nyingi za wilaya ili kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi, ambapo hadi sasa tumeongeza mtandao wa barabara za wilaya kutoka kilomita 108,946.19 hadi kufikia kilomita 144,429.77.
“Hadi Juni, 2024 barabara za lami za wilaya zilikuwa kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31, kati ya hizo, kilomita 2,743.81 zipo katika hali nzuri, kilomita 445.18 zipo katika hali ya wastani na kilomita 148.68 zipo kwenye hali mbaya“ amejinasibu Mhandisi Seiff.
Pamoja na mambo mengine Seiff amezungumzia kuhusu ujenzi wa Daraja na uendelezaji wa mto Msimbazi, ambapo eneo la chini la mto huo linatarajiwa kuongezwa kina na kutanuliwa ili kuruhusu maji kwenda baharini kwa kasi inayotakiwa.
Amesema mradi huo ulioanza rasmi Februari 16,2023 ambao unatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola za Marekani Milioni 200), Serikali ya Hispania (Euro Milioni 30) na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi
Kuhusu fidia Mhandisi huyo amesema “Hadi sasa asilimia 98 ya watu ambao wanaathirika na mafuriko wamelipwa fidia na wameondoka, lakini pia zipo takribani Maya 314 ambazo zimetambuliwa kuwa zitaathirika na ujenzi na mchakato wa kuandaa daftari la fidia ambao utaanza mwezi huu wa Septemba”





