NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Huduma za Kibenki Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Agathon Kipandula amesema kuwa BoT inawajibu wa kuikopesha serikali mkopo wa muda mfupi usio wa kibajeti wa asilimia 18.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kipandula amesema kuwa mkopo wanaotoa kwa serikali upo kwa mujibu wa sheria sura ya 197 ya mwaka 2006 na mwamba serikali imekuwa ikilipa madeni.
Kipandula amesema kuwa utaratibu unaofanyika ni kwa benki kuu zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani kwani wote wanatumia sheria moja na kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo, benki hiyo inatunza fedha za serikali zote mbili na mashirika ya umma hivyo, pale wanapokuwa na uhitaji huwakopesha.
Amesema kuwa kwa sababu ya kuwa na mteja ambaye ni serikali, sheria hiyo imetoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa lengo la kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya serikali.
‘’Sheria hii pia imeweka ukomo wa kukopa ambao kwa mujibu wa sheria ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka jana,’’ amefafanua Kipandula.
Ameongeza kuwa “kwa mambo ambayo yanaendelea, sheria inatusimamia katika kuendesha shughuli za serikali ikiwemo kutoa huduma ya mkopo wa muda mfupi kuziba pengo au nakisi.’’
Kipandula amesema sheria hiyo inaitaka serikali kuchukua mkopo huo usio wa bajeti, ndani ya siku 180 na kwamba kila mwisho wa mwezi serikali inarudi katika nafasi yake na kurejesha mkopo huo.
“Mkopo huo sio ule ambao tunadetermine amount kwamba watakopa kiasi hiki, huu unabalance cash flow yake kwamba kama leo anajukumu la kulipa Sh. 10,000 na alizo nazo ni Sh. 5,000 basi Sh. 10,000 itakuja kama overdraft na akipata fedha zake basi atarudisha.’’ amesema
Amesisitiza kuwa si kweli kwamba serikali ilikopeshwa kiasi cha fedha na BoT kwa aina tofauti kwani hata kwenye vitabu vya serikali hakuna kiasi hicho.
Aidha, amesema kuwa mkopo wa aina hiyo hauhitaji kupitishwa na bunge isipokuwa wataonesha kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
‘’Kulikuwa na taarifa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Fedha ameshalitolea ufafanuzi, tunachokieleza hapa ni kuongeza uelewa wa masuala yanayoendelea BoT’’ amefafanua