NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi atatoa hotuba ya ufunguzi wa maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba kwa kutumia lugha ya Kiswahili kesho
Ameyasema hayo leo Julai 2,2024 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumkaribisha Rais Nyusi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu.
Kesho Jumatano Julai 3, 2024 Rais Nyusi atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba na atasindikizwa na mwenyeji wake Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa hayo yanafanyika ni kutokana kwamba watu wa nchi hizo mbili wanaongea lugha zinazoelewana.
“Rais Nyusi akizungumza kimakonde, Wamakonde waliopo Mtwara pale watamuelewa na kujua nini amesema, Tamaduni zetu pia zimetuunganisha na hayo ndio yametufanya tuwe wamoja katika kufanya biashara, uwekezaji, kuona, na kufanya Msumbiji kuwa siyo tu nchi jirani kwa Tanzania bali ni ndugu na rafiki wa siku zote,” amesema .
Amesema urafiki wa nchi hizo mbili uliwekwa vizuri na baba wa mataifa hayo mawili ambao ni Hayati Edward Mondlane na Mwalimu Julius Nyerere wakati ule nchi hizo zikitafuta uhuru kutoka kwa Wakoloni.