NA TERESIA MHAGAMA, IFAKARA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko
amezindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (
20MVA) ambacho kukamilika kwake kumesavabisha Wilaya za Kilombero,
Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro kupata umeme wa kutosha na wa
uhakika.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho wilayani Kilombero
Mkoa wa Morogoro leo Mei 31,2024 ,Dk. Biteko amesema kuwa mradi huo una manufaa
mbalimbali ikiwemo kuboresha upatikanaji umeme kwenye wilaya hizo,
kuwezesha uwekezaji zaidi wa viwanda hasa vya kilimo kama vile mpunga,
kupeleka huduma kwenye taasisi ikiwemo vituo vya afya na Shule na
kuongeza wigo wa gridi ya Taifa.
“ Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan
inachukulia kwa uzito mkubwa suala la upatikanaji wa nishati kwenye
maeneo yetu, wimbo wetu Wizara ya Nishati si kusema maneno mengi bali
kupeleka umeme kwa wananchi, umeme kwetu si anasa bali ni jambo la
lazima.” amesema Dk.Biteko
Amemshukuru Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za
kuwezesha mradi huo ulioanza mwaka 2020 ambapo fedha za kutekeleza
mradi takriban shilingi Bilioni 25 zimetolewa na Serikali ya Tanzania
pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).
Aidha, DBiteko amewataka Watendaji wa TANESCO na REA kufanya kazi
kwa ufanisi na weledi ili kuweza kufikisha umeme wa uhakika kwa
wananchi.
“ Napenda kuwapa hamasa wote mnaohusika na Sekta ya Nishati (REA na
TANESCO) kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi hii muhimu
itakayochochea kukua kwa uchumi wa watu wetu na niwatake muimarishe
usimamizi wa miradi hii ili iendane sawa na thamani ya fedha
zinazotolewa.” amesema
Amesema uwepo wa kituo cha umeme Ifakara unaenda kuchochea uwekezaji
ikiwemo ufunguaji wa viwanda 54 vya kuongezea thamani mazao, ujenzi wa
migodi mikubwa unaoendelea wilayani Ulanga ambayo ilikuwa ikihitaji
umeme wa uhakika ambapo amesema Serikali imeamua kujenga laini ya
umeme km 68 kupeleka umeme kwenye migodi hiyo kwa thamani Sh. Bilioni
104.
Katika hatua nyingine Dk Biteko amesema Serikali itafungua Ofisi ya
TANESCO ngazi ya Mkoa kwenye Kanda ya Morogoro Kusini ili kusogeza
huduma zake kwa wananchi badala ya kutegemea kupata huduma kutoka
Ofisi ya Mkoa iliyopo Morogoro mjini.
Ameishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa kuiunga Serikali katika
utekelezaji wa mradi huo na kuiomba Jumuiya hiyo kushirikiana na
Serikali kuongeza transfoma nyingine kwenye eneo la Kituo cha Ifakara
ili kuongeza zaidi nguvu ya umeme ambao pia utaingizwa kwenye gridi ya
Taifa.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Christine Grau ameipongeza
Wizara ya Nishati, REA, TANESCO pamoja na Wakandarasi kwa
kukamilisha mradi huo ambao unaenda kubadilisha maisha ya wananchi
kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa Tanzania na Umoja wa Ulaya zimekuwa na ushirikiano wa
muda mrefu katika masuala ya Nishati kwa kuwa ndiyo injini katika
kuleta maendeleo endelevu na ushirikiano huo umejikita katika maeneo
mbalimbali ikiwemo Nishati Safi ya Kupikia.
Ameeleza kuwa mradi huo wa Ifakara umewezesha wananchi pamoja na
taasisi kupata umeme wa uhakika na kwamba wananchi watatumia umeme huo
kujiendeleza kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani
mazao yao.
Ameahidi kuwa EU itaendele kuiunga mkono Tanzania ya Nishati ili
wanannchi wapate Nishati ya uhakika.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amempongeza Rais, Dk. Samia
Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi ambao unaonekana kwa namna
mbalimbali ikiwemo upelekaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi.
Ameongeza kuwa awali wilaya hizo zilikuwa zikipata umeme mdogo na
kufanya huduma nyingi kutopatikana kwa ufanisi lakini sasa uwepo wa
umeme wa uhakika utapelekea uanzishaji wa viwanda vidogovidogo ikiwemo
vya ukoboaji mpunga kwa kuwa eneo hilo ni mzalishaji mkubwa wa mpunga
nchini.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
Mhandisi Jones Olotu alisema kuwa, REA ilijenga kituo hicho kutokana
na kuwa eneo la kimkakati kutokana na uzalishaji wa mpunga na migodi.
Amesema kuwa jumla ya Wateja 1858 wameungwa na umeme kupitia mradi huo
katika vijiji 8 vya Wilaya ya Kilombero, hii ikijumuisha Shule,
Zahanati, Vituo vya Afya, Vituo vya Watoto Yatima, Makanisa na
Misikiti.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga ameshukuru
kwa uwepo wa kituo hicho pamoja na umeme kufika kwenye vijiji vyote
Wilaya ya Kilombero ambapo ameomba umeme huo ufike vitongojini.