- HII bahasha ya kaki, kweli inatoa utu,
Mambo yenye unafiki, hayo yayafanya kwatu,
Kwa kuwa inabariki, yale wamejaa kutu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha haki. - Ilikuwepo zamani, na sasa wafanya watu,
Pale palipo amani, na mambo yaliyo haki,
Inacholeta uhuni, na kusababisha chuki,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha haki. - Kwake Pontio Pilato, waliitumia watu,
Yuda lifanya kipato, kwa kumsaliti mtu,
Wakapita ya mkato, kwa ile yao papatu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha haki. - Alipofufuka Yesu, wakapewa rushwa watu,
Waseme yasiyohusu, kufufuka kuwe butu,
Pesa walivyoibusu, uongo ukawa kwatu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha haki. - Kutoa haki ni rushwa, wanalalamika watu,
Hata kazini ni rushwa, watu hawajali kitu,
Kwenye elimu ni rushwa, wapunjwa wana wa watu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha watu. - Michezoni nako rushwa, wanalalamika watu,
Sheria zinapindishwa, sababu ya hicho kitu,
Maamuzi kupindishwa, na kukasirisha watu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha watu. - Ni muda wa kuamshwa, kusinzia sio utu,
Tuoneshe tumechoshwa, kwa haya matendo yetu,
Tusisubiri kuoshwa, nayo TAKUKURU yetu,
Rushwa angalia Rushwa, inavyopotosha watu. - Kuweza kuendelea, tuonekane ni watu,
Bora haki pendelea, wala si rushwa ya vitu,
Uchumi tutachochea, kwa maendeleo yetu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha watu. - Hata kwa michezo yetu, ihusuyo timu zetu,
Haki iwe ndiyo yetu, kwa maendeleo yetu,
Rushwa isitajwe kwetu, kifo cha michezo yetu,
Rushwa angalia rushwa, inavyopotosha watu.
10.Kweli ipate tawala, katika matendo yetu,
Tusipende kulakula, kujaza matumbo yetu,
Hilo onyo si mkwala, latuhusu sisi watu,
Rushwa ngalia rushwa, inavyopotosha watu.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602