- NANI anawakumbuka, ni kama wapo yatima,
Hao wanachakarika, kwa yao nyingi hekima,
Na hata wao hufika, kukosa muda wa vyama,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Japo wote wahusika, chekechea hadi chuo,
Nataja walohusika, kwa kutuvalisha nguo,
Hawakuwa wanadeka, kwa mapozi ya vituo,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Ujinga hadi kufika, kusoma na kuandika,
Ni kazi kubwa hakika, ipasayo kusifika,
Yatufanya tunawaka, nafasi nyingi twashika,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Sisi tuliozeeka, chekechea siyo yetu,
Msingi tunakumbuka, ndizo zilikuwa zetu,
Asubuhi tulifika, kwa walimu wenye utu,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Utu wetu mmeshika, hata kama hamtajwi,
Jisikieni hakika, wala nyie si mazimwi
Kila anayesifika, nyie japo hamsemwi,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Wachache nawakumbuka, walionifunza kwanza,
Ni walimu watukuka, hadi leo wapendeza,
Kama kwenu nasikika, pongezi ninaongeza,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Walimu mmetukuka, wmatupatia maisha,
Elimu tumeishika, ndio inatuamsha,
Ya afya tunayashika, na maji tunachemsha,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Bila nyie tungechoka, ujuzi tusingepata,
Tungebaki na machaka, maradhi yangetupata,
Hatua tusingevuka, tungebaki kutepeta,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Weledi ukiutaka, ni sababu ya walimu,
Ujinga unaponyoka, unapata ufahamu,
Hapo hata ukitoka, unakuwa mtaalamu,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Pongezi zisompaka, zifike kwenu walimu,
Jinsi mnavyotuoka, mwatufanya wanadamu,
Ona tunatajirika, na kuweza kujikimu,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Ombi kwenu wasifika, mnaomiliki shule,
Waondolee mashaka, walimu wetu wapole,
Kipato wapate shika, na chakula chao wale,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa. - Tunakuomba Rabuka, uwalinde waalimu,
Waishi bila mashaka, na kazini wakidumu,
Sote tufike mpaka, ng’ambo Bahari ya Shamu,
Tuwashukuru walimu, wametufikisha hapa.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB) 0767223602