- ULIMI kama shilingi, kwa zile tabia zake,
Huku alama ni nyingi, kwingine ziko za kwake,
Unayo mazuri mengi, na mabaya pia yake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Salamu ni kwa ulimi, pia na matusi yake,
Heshima ni kwa ulimi, hata dharau ni yake,
Huu hauna usomi, unajifanyia yake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Mama kazaa mtoto, kutoka tumboni mwake,
Amtukana mtoto, kama siyo binti yake,
Afanyao ni utoto, ulimi wafanya yake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Baba miaka sitini, atongoza binti yake,
Mke kamwacha nyumbani, afanya maombi yake,
Hajui wake mwandani, anafuja ndoa yake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Unadanganya naona, wasema shauri yake,
Hujui Mungu aona, unayo adhabu yake,
Ulimi unajivuna, umefanya mambo yake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Pande mbili za shilingi, hiyo ni asili yake,
Ukweli uongo mwingi, ni chukizo mbele yake,
Uvuguvu ni mwingi, hauna nafasi kwake,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Mungu atusaidie, kwa vizuri tusomeke,
Ulimi tuutumie, kwa Mungu tukubalike,
Wala tusijifanyie, kinyume tuadhirike,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Kama maneno wasema, wasikiao wacheke,
Pengine hiyo alama, kwako na ifahamike,
Vile wanavyokusoma, hukupaswa usikike,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Ulimi wako kisema, watu wote waitike,
Wanajua wewe mwema, ni vizuri usikike,
Kesho mabaya kitema, tafanya uadhirike,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema? - Ulimi kiungo chema, ni vizuri kitumike,
Sio kupanga hujuma, za watu wapukutike,
Ulimi uteme mema, hata Mungu aridhike,
Tuuchungeje ulimi, tuishi maisha mema?
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602