- HEBU salimia watu, pesa zitakuishia,
Sema vizuri na watu, kazi ni ya kufikia,
Heshimu vizuri watu, cheo tumekupatia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Tunaishi nao watu, pesa wanajivunia,
Bila pesa siyo mtu, vile wanakusagia,
Hawajui sisi watu, kaburini twaishia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Pesa zanunua vitu, mtaani watambia,
Lakini si kama mtu, utu twaufagilia,
Kamwe sikufanye mtu, wengine kuwasagia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Pesa tambia viatu, vile tunakanyagia,
Usiwadharau watu, waloumbwa na Jalia,
Jua wajipaka kutu, bora haya kisikia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Kazi wanafanya watu, mwishoni inaishia,
Isijekufanya katu, wengine kuwanunia,
Itakatika kazi tu, sitini ukifikia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Kazi kipimo cha utu, wahenga watuambia,
Hivyo kuheshimu watu, heshima wajipatia,
Lakini dharau watu, utakuja kujutia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Cheo hukaa mtu, sisi kututumikia,
Usije kufanya watu, kukupa wakajutia,
Waheshimu hao watu, ndiko utakoshukia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Haya maisha ya watu, ngazi tofauti pia,
Wenye nacho hao watu, na wasionacho pia,
Wanachofanana utu, ndio wakuheshimia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja. - Twapumua sote watu, chakula twakula pia,
Tunalala sote watu, na mwishowe twajifia,
Katu hatwendi na kitu, vyote hapa vyasalia,
Bora kuheshimu utu, huo hauna daraja.
Na Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602