ADILI YA MALENGA
1.MOSHI haiwezekani, mu wenyewe kila mwaka,
Tukaribishe wageni, kwenu tuweze kufika,
Mjini na vijijini, tuone mwashereheka,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
2.Noeli i mdomoni, wengi wamekwishafika,
Wengine wako njiani, kwenda kuufunga mwaka,
Hao waenda nyumbani, huko kunatamanika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
3.Koo na koo nyumbani, jinsi wanajumuika,
Ya kwao yale ya ndani, kwa wao yafahamika,
Lakini sisi wageni, wafanyayo yatushika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
4.Kuolewa uchagani, ujue unahusika,
Ukioa uchagani, na wewe utahusika,
Mila ya kwenda nyumbani, huko sana yatukuka,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
5.Tusikiavyo wageni, huko nyama zinalika,
Siku zote shereheni, ndugu wanajumuika,
Na hata makanisani, misikiti wafurika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
6.Kote waliko nchini, nyumbani wakusanyika,
Wazazi walo nyumbani, kipindi wafurahika,
Wakumbushana zamani, mengi yaliyowafika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
7.Hata walo ugenini, Ulaya na Afrika,
Disemba wako nyumbani, na ndugu kujumuika,
Na watoto wao ndani, wote wanakutanika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
8.Ni bora utamaduni, kurudi tulikotoka,
Kujifunza ya nyumbani, ingawa tulishatoka,
Huko tusiwe wageni, ulazima ukifika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
9.Furaha sasa nchini, ya Wachaga tunadaka,
Kwa sasa wengi nchini, nyumbani wajumuika,
Wanafika mashinani, kule kule walitoka,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
10.Vizuri kwenda nyumbani, huko ndiko tulitoka,
Tukikutana nyumbani, watoto wakihusika,
Wawajue wa nyumbani, na wengine wahusika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
11.Sherehe njema jamani, tukimalizia mwaka,
Itutawale amani, kote tukishereheka,
Tuweze fika mwakani, sote tukifurahika,
Kitu ninachokienzi, hawa ndugu kwenda kwao.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com