SERIKALI ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na ile ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) inayoongozwa na Felix Antoine Tshisekedi Tshilombo zimefuta Viza kwa raia wake.
Maana yake ni Lwamba raia wa mataifa hayo mawili sapo huru kusafiri kuingia kwenye nchi hizo bila kuwa na vikwazo vya muda wa kukaa.
BBC Swahili imeripoti kuwa kwa mujibu wa takwimu za makadirio za Umoja wa Mataifa hadi kufikia 2023, DR Congo ina watu wanaokadiriwa kuwa milioni 102, ni taifa la nne Afrika kwa kuwa na watu wengi nyuma ya Nigeria, Ethiopia na MisriEgypt. Na la 15 ulimwenguni kuwa na idadi kubwa ya watu.
Licha ya Tanzania na DR Congo kupakana, pia raia wa nchi hizo wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili. Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania ni wazungumzaji wa Kiswahili. Upande wa DR Congo kuna wazungumzaji wa lugha hiyo wanaokadiriwa kufika 40% ya watu wake hasa wale wanaopakana katika mikoa ya Mashariki ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa nchini Tanzania ya mwaka 2020, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ndio inayoshika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi jirani kupitisha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, DR Congo hupitisha zaidi ya 30% ya mizigo yote.
Kutoka 2018 upitishaji huo umezidi kuongezeka, 2018 DR Congo ilipitisha tani milioni 1.8, 2019 tani milioni 1.9, 2020 tani milioni 1.8, 2021 tani milioni 2.4 na 2022 tani milioni 3.4.
Katika juhudi za kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba alieleza mwezi Agosti mwaka huu kuwa Tanzania inatafuta eneo kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupatiwa bandari kavu ya kuhifadhia mizigo ya nchi hiyo.
Kauli hiyo ilikuja baada ya mazungumzo na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ekila Libombo, kuhusu mipango ya kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kati ya nchi hizo ili kukuza biashara na uchumi.
Mbali na bandari ya Dar es Salaam, mkoa wa Kigoma – uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania karibu na fukwe ya Mashariki ya ziwa Tanganyika – pia ni lango kuu la kibiashara kati ya Tanzania na DR. Congo.