NA MWANDISHI WETU, GEITA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ameipongeza Serikali kwa kujenga shule mpya 80 katika mkoa wa Geita.
Katibu Mkuu ameyasema hayo wakati akihutubia kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Wilaya ya Bukombe mara baada ya kupokea taarifa ya mradi wa ujenzi na kushiriki uzinduzi wa Ukumbi, Nyumba ya kupumzikia Wageni (Rest House) na Jengo la Mgahawa (Restaurant) katika Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe ambapo hadi sasa zimeshatumika zaidi ya fedha za Kitanzania shilingi milioni 200.
“Nipongeze sana Serikali kwa mkoa mmoja tu wa Geita ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili zimejengwa shule mpya 80 sio jambo dogo” alisema Chongolo.
Pamoja na mambo mengine Katibu Mkuu amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu ameongozana na Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Ussi (Gavu) ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Geita.