NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kuacha mtindo wa kusubiri vikao vya baraza kuwasilisha kero na changamoto za wananchi, badala yake watumie ofisi yake ambayo ipo wazi wakati wote kufikisha kero za wananchi.
Meya Mwamfupe alisema hayo wakati wa kikao cha kawaida cha robo ya tatu ya mwaka cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jijini hapo.
“Milango ya ofisi yangu ipo wazi kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko na kero za wananchi, badala ya kusubiri vikao vya madiwani vinachofanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu,” alisema.
Mwamfupe ambaye pia ni diwani wa Kata ya Madukani katika jiji hilo alisema, madiwani wote wa kata 41 za jiji hilo, wamekuwa hawatumii fursa ya uwepo wazi ofisi yake, kitendo ambacho kimejionesha wakati wa maswali ya papo kwa hapo ya madiwani, yote yaliyoulizwa zilikuwa kero za muda mrefu za wananchi ambazo zingekuwa zimetatuliwa bila kusubiri baraza.
Kero nyingi za wananchi, hazitakiwi kusubiri kikao cha madiwani, zingeweza kupatiwa ufumbuzi mara moja kupitia ofisi yake.
Katika kuharakisha utatuzi wa kero za wananchi ataweka daftari katika ofisi za jiji ili kuwapa nafasi madiwani hilo kufika na kuandika kero za wananchi badala ya kusubiri vikao vya baraza vinavyofanyika mara nne tu kwa mwaka.
Akiunga mkono kauli ya Meya Mwamfupe kuhusu madiwani kuwasilisha changamoto na kero za wananchi kila wakati, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema ofisi ya wilaya pia inatoa kipaumbele kwa madiwani kufikisha changamoto na kero za wananchi wakati wote, hivyo watumie fursa hiyo.
Akijibu baadhi ya kero za wananchi zililoulizwa katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo, hasa kuhusu hatua zinazochukuliwa na jiji kudhibiti mtindo wa bajaji na bodaboda kuegesha hovyo kila mahali katikati ya jiji, Mkuu wa Divisheni ya Rasilimaliwatu na Utawala Francis Kilawe kuhusu uegeshaji bajaji hovyo kati ya jiji alisema, mgambo wa jiji wataanza kuzikamata na kutoza faini kubwa.
Mwamfupe alisema changamoto kama hizo za uegeshaji mbaya kati ya jiji hazitakiwi kusubiri vikao vya baraza la madiwani, bali zinaweza kufikishwa ofisi kwake kila wakati.