NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KAMISHNA wa Mipango ya Kitaifa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Mursali Milanzi amesema kuwa ni muhimu kuwekeza katika rasilimali watu kwani huko ndiko wanapopatikana wataalam wenye ujuzi na uelewa wa kutosha ambao watasaidia kusimamia masuala ya maendeleo nchini.
Dk. Milanzi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano uliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kuwakutanisha wadau walioandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na watakaoandaa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Dk. Milanzi amesema kuwekeza katika rasilimali watu ni kitu muhimu ambacho wanatamani kuwepo katika dira mpya ya maendeleo ya Taifa 2050 na kwamba jambo hilo likifanikiwa watapatikana wataalam wenye ujuzi ambao watasimamia vema maendeleo na kufanya nchi kupiga hatua na uchumi wake kukua.
“Pia jambo ambalo tunapaswa kulifikiria sasa katika dira mpya ya maendeleo ya Taifa 2050 ni kufanya mabadiliko ya kiuchumi na uwe wa kisasa na sekta zote ikiwemo kilimo zibadilike na ziwe za kisasa, mfano tunapokwenda miaka 25 ijayo hatuwezi kuzungumza kilimo cha huko nyuma.
“Sekta hii ya kilimo ikiwa ya kisasa itaongeza tija, hivyo masuala ya kutumia mbegu na umwagiliaji unapaswa kuwa kisasa na hilo ndilo jambo tunapaswa kulifikiria katika dira mpya ya 2050, tunaweza kupata maendeleo makubwa kama tutaelekea upande huo,” amesema Dk. Milanzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Maandalizi ya dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050.
Hata hivyo amesema kama sekta zote za uzalishaji na kijamii kama elimu na afya zikifanywa nazo kuwa za kisasa zaidi nchi itaweza kupiga hatua kubwa katika masuala yote ya maendeleo.
“Watanzania wamekuwa wakipiga kelele kuhusu maendeleo, kikibwa hapa ni namna gani tunawaongoza kufikia hayo maendeleo hivyo tukiwa na dira ambayo ipo wazi na kila mtanzania akaielewa vizuri mimi naamini kabisa watasaidia kwenye kukimbiza huo mchakato wa maendeleo,” amesema
Awali akifungua mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema wamewakutanisha wadau hao ili wafanye uchambuzi wa mafanikio na kuangali changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa dira inayokwenda kuisha muda wake miaka miwili ijayo.
“Hii ni mipango mikubwa na maamuzi mazito ya kitaifa kwahiyo haiwezi kuchukuliwa kirahisi rahisi ndio maana tumewaita wadau mbalimbali, kwani tunafahamu kuwa taifa lolote duniani linakuwa na mpango wa muda mfupi, wa kati na mrefu, huu ni mpango wa muda mrefu ambao maamuzi yake yataathiri vizazi vijavyo,” amesema
Aidha Singo amesema taasisi ya Uongozi iliona ni muhimu kuwakutanisha wadau hao ili kuja kuzungumza kwa uhuru kipi ambacho kinafanya kazi na hakifanyi kazi katika utekelezaji au uaandaaji wa mipango hiyo ya maendeleo.