NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) kimetangaza maandamano ya amani kushinikiza wabunge 19 waliopo bungeni ambao walifukuzwa uanachama waondolewe bungeni
Mratibu wa uhamasishaji wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Aisha Machano amesema baraza lake limejiandaa kufanya maandamano yasiyo na kikomo mpaka pale wabunge hao 19 watakapoondolewa bungeni.
Katibu wa kamati ya maandamano, Celestine Simba ametangaza kuwa maandamano hayo yataanza kufanyika Jumanne, Mei 9 ambapo wanawake wa chama hicho wataelekea ofisi ndogo za bunge zilizopo jijini Dar es Salaam.
“Tumeshaandika barua kuwataarifu Polisi juu ya maandamano hayo. Tutaanzia makao makuu ya chama na tutaelekea ofisi ndogo za bunge.
“Tutajipa muda kidogo na kama Spika wa Bunge Tulia Ackson hatawafukuza wabunge hao, basi maandamano yatahamia jimboni kwake, Mbeya mjini ambapo tutakwenda kumshtaki kwa wananchi,” amesema Simba
Katibu huyo wa kamati ya maandamano amesema baada ya maandamano ya Dar es Salaam, watahamia Mbeya mjini jimboni kwa Spika Tulia kisha watahamia mjini Dodoma kufanya maandamano kama hayo kushinikiza wabunge hao 19 waondolewe bungeni.