NA MWANDISHI WETU, TANGA
SERIKALI kupitia wizara ya Maji imeeleza mpango mkakati wa kuhakikisha unatatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani kupitia mradi mkubwa wa kutoa maji ya mto pangani na kuyasambaza katika maeneo hayo ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 171.
Hayo yamebainishwa na waziri wa Maji Juma Aweso Aprili 16, 2023 katika ziara yake ya siku moja wilayani Korogwe iliyolenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo.
” Tunampango mkakati wa kutoa maji katika mto Pangani na kusambaza katika wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani ili kuhakikisha wanatumia mto huo kupata maji safi na salama” alisema Aweso
Aidha Aweso ameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wakiwa wanasubiri kukamilika kwa mradi huo mkubwa ambao utaenda kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo ikiwemo uchimbaji wa visima zaidi ya saba.
“Jitihada ambazo tumezifanya za muda mfupi ni uchimbaji wa visima ambavyo vitaweza kuingizwa kwenye mfumo ili wananchi wa Korogwe waweze kupata huduma ya maji safi na salama wakati wanasubiri mradi ukamilike” aliongeza Aweso
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya korogwe Jokate Mwegelo ameipongeza Serikali kwa hatua waliyochukua katika kuhakikisha wananchi wa Korogwe wanapata huduma ya maji safi na salama kwa akihakikisha wanasimamia kwa ukaribu maagizo yote yaliyotolewa katika kutekeleza mradi huo ambao utaenda kutatua tatizo la maji wilayani humo.
“Tutaendelea kuhakikisha watumishi wa maji wanatimiza wajibu wao tunafahamu maji ni uhai na kiu kubwa ya wananchi wa korogwe ni kuona adha ya maji inatokomea” alisema Mwegelo