NA MWANDISHI WETU, TANGA
MKUU wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa, ametoa msaada wa vyakula kwa vituo vitatu vya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Msaada huo ameutoa wakati wa futari ambayo ameiandaa nyumbani kwake, ambayo imehusisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na viongozi mbalimbali wa kidini na serikali.
Amesema kuwa watoto hao ni sehemu ya jamii, hivyo wanahitaji kupatiwa faraja, ili nao wasione wametengwa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea sherehe za sikukuu ya Idd.
“Mara nyingi kundi hili la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na walioko kwenye vituo huwa wanasahauliwa, hivyo niwaombe wananchi na jamii kuwakumbuka kwa kuwapatia misaada mbalimbali, ambayo itakuwa ni sehemu ya faraja kwao,”amesema.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Jumaa Luuuchu amesema kuwa katika kipindi hiki cha mfungo ni muhimu waumini kufanya matendo mazuri ya kumpendeza mungu, ikiwemo kuomba toba, ili nchi iweze kuendelea kuwa salama.