NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
WAHITIMU 22 kutoka nchini Kenya wametunukiwa vyeti vya kozi ya muda mfupi ya Cargo Tallyingi for International Shipping inayohusika na kuhudumia shehena ndani na nje ya nchi.
Wahitimu hao wametunikiwa vyeti hivyo na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) baada ya kuhitimu na kufanya vema katika masomo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 6, 2023 mara baada ya kuwatunuku vyeti wahitimu hao, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kaimu Mkeyenge amesema, sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji imepiga hatua katika ukanda wa Afrika Mashariki hivyo amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kusoma kozi za kuhakiki shehena zinapotoka na kuingia nchini.
Amesema sekta hiyo imepiga hatua katika ukanda wa Afrika Mashariki hivyo ni muhimu kuwa na wataalamu wa kutosha watakaokuwa na uwezo mathubuti wa kuhudumia eneo hilo.
Aidha amesema kuwa madhumuni ya kozi hiyo fupi ni kuwajenga vijana kuwa wahakiki wazuri wa shehena zinazotoka nchi za nje kuingia ndani ya nchi za Afrika Mashariki ikiwa pamoja na zile zinazotoka nchini kwenda nchi nyingine kwa kupitia vyombo vya usafiri kwa njia ya maji.
“Hii ni moja ya mpango wa kubadilishana wakufunzi na wanafunzi katika eneo la kanda ya Afrika Masharikii ni katika kutekeleza mradi unaendeshwa na benki ya dunia katika vyuo vilvyopo katika kanda yetu,” amesema
Amesema kuwa kozi hiyo ya mwezi mmoja ina kwenda kuwafanya kuwa wafanyakazi wazuri katika maeneo ya bandari na uingizwaji na utolewaji wa shehena lakini pia katika maeneo ambayo ufungwaji wa shehena unafanyika katika maeneo ya bandari.
Aidha Mkeyenge amesema kuwa wanafunzi wengine wanatarajiwa kupokelewa kwajili ya kubadillishana uzoefu na mafunzo huku na wanafunzi wa hapa nchini wataenda katika vyuo vya nchi nyingine kwaajili ya mafunzo hayo.
Amesema kuwa ushirikiano huo unasaidia kukuza uchumi wa kikanda kupitia njia ya usafiri kwa njia ya maji pia ushirikiano huo utawezesha kufanya biashara za kikanda bila kutegemea nchi nyingine.
Kwa upande wa Mkuu wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa amesema kuhitimu ya wanafunzi hao 22 ni zao la kwanza tangu kuanzishwa kwa kituo cha umahari wa usafiri wa anga na operesheni za usafirishaji chuoni hapo.
Amesema katika mradi wa benki ya dunia vituo vya Umahiri vipo 16, kwa Tanzania vipo vinne ikiwa kimojawapo kipo NIT ambacho kimewatunuku vyeti vyao wahitimu 22 kutoka nchini Kenya.
Kwa nchini Kenya vituo vya umahili vipo vitano na Ethiopia vipo vituo sita (7) ambavyo vinawezesha wakufunzi na wanafunzi kubadilisha ujuzi na mbinu za ufundishaji.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mhitimu, Victor Omondi waliohitimu mafunzo hayo ya mwezi mmoja kutoka Chuo cha Kenya Coast National Polytechnic (KCNP) Mombasa amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza taaluma na ujuzi wa wanafunzi katika vyuo vinavyonufaika na ufadhili huo.