MANHATTAN, MAREKANI
POLISI katika miji mikuu ya Marekani wanajiandaa kwa ghasia zinazoweza kutokea leo Jumanne, Machi 21, 2023 iwapo Rais wa zamani Donald Trump atakamatwa wiki hii kama sehemu ya uchunguzi wa pesa aliyotoa kama rushwa.
Mwendesha mashtaka wa Manhattan anaweza kumshtaki Trump kwa madai kwamba alimlipa pesa mcheza filamu za ngono Stormy Daniels, ili kumnyamazisha asizungumzie mahusiano wanayodaiwa kuwa nayo.

Vizuizi vya chuma tayari vimewekwa tangu jana Jumatatu nje ya Mahakama ya Jinai ya Manhattan, ambapo Trump atashtakiwa, kuchukuliwa alama za vidole na kupigwa picha iwapo mashtaka yatawasilishwa wiki hii, kama vyombo vya habari vya Marekani vilivyoripoti
Wiki iliyopita Trump alitoa wito kwa wafuasi wake kupitia mitandao ya jamii akipinga hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.
Mmoja wa mawakili wa Trump alisema madai hayo yalitokana na ripoti za vyombo vya habari kwamba anaweza kufunguliwa mashtaka leo Jumanne.
Iwapo Trump atashtakiwa, itakuwa kesi ya kwanza ya jinai kuwahi kufikishwa mahakamani dhidi ya rais wa zamani wa Marekani.

Pia italeta athari kubwa kwa kampeni yake ya kuwa mgombea wa urans kupitia chama cha Republican katika uchaguzi wa rais ujao wa mwaka 2024
Kwa miaka mitano, waendesha mashtaka mjini New York wamekuwa wakichunguza madai ya kashfa hiyo kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2016.
Mcheza filamu huyo, Daniels anasema alilipwa Dola za Kimarekani 130,000 (sawa na sh. 304,221,295 za Kitanzania) na aliyekuwa wakili wa Trump, Michael Cohen kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016 kama njia ya kunyamazisha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Trump alikanusha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na amesema ni kesi inayotengenezwa mahasimu wake kisiasa.