NA THOMPSON MPANJI, MBEYA
WAKAZI wa Kata ya Sisimba,jijini hapa wametaja baadhi ya kero kubwa sita ambazo wamedai hazijashughulikiwa kwa muda mrefu hali inayowarudisha nyuma kiuchumi kupitia shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo na kujiona kama wametelekezwa nyikani ama kisiwani.
Aidha wakazi hao wamelalamikia utaratibu uliotumika kuwachagua baadhi ya wanufaika wa mfuko wa TASAF ikiwemo Bima ya Afya inayodaiwa kutolewa kwa huruma ya Mbunge wa Mbeya Mjini,Dk Tulia Ackson Mwansasu kuwa baadhi ya viongozi waliopewa jukumu la kugawa msaada huo, hawakuzingatia usawa wala vigezo vinavyohitajika kuwatambua wahusika.
Hivi karibuni Mbunge wa Mbeya Mjini Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,alitoa msaada wa kadi ya Bima za Afya kwa baadhi ya wananchi ambao hawajiwezi kugharamia huduma ya Afya katika Kata 36 jijini hapa ili waweze kuzitumia kwa muda wa mwaka mmoja.
Wakizungumza na Demokrasia kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi hao wamesema kuwa Serikali inapaswa kuchukulia umuhimu na uzito wa kipekee kero sugu zinazowakabili kabla hawajapa hadhi ya kuwa Jiji.
Wametaja baadhi ya kero hizo ni pamoja na kukosekana kwa Kivuko cha juu kwa watembea kwa miguu katikati ya eneo hatari na korofi la Mwanjelwa na Kabwe,Barabara za mitaani zitakazoweza kusaidia kupunguza msongamano wa barabara kuu ya Tanzam,ujenzi wa mifereji ya kutoa maji ,ujenzi wa maghuba ya taka,Soko la Uhindini sanjari na taa za barabarani.
Johnson Mwasote, pamoja na Esther Sikanyika wakazi wa maeneo ya Mwanjelwa wamesema kuwa licha Mbeya kupewa hadhi ya Jiji lakini huduma zake haziendani ya sifa hiyo ambapo wakazi wake wamekuwa wakikosa huduma za msingi .
“Leo hii Mbeya mvua zinavyonyesha unaona maji yanavyopita barabarani yakiwa wamezoa taka kutoka sehemu moja na kupeleka barabarani…hakuna mifereji ya kupitisha maji kumwaga katika mito iliyopo katikati ya Jiji,ukiingia Mbeya usiku unakutana na kiza,angalia pale Mwanjelwa na Kabwe kuvuka kuelekea upande wa pili ni shida kutokana na msongamano wa magari…panahitajika kivuko cha kupita juu..”wamesema.
Mwasote ametaja kero nyingine inayohitaji kuchukua hatua za haraka ni pamoja na kukosekana kwa katika eneo la Uhindini baada ya Soko lililokuwepo kuteketea jambo ambalo amedai lillikuwa likiongeza mzunguko wa fedha na kuuchangamsha Mji wa Mbeya.
Katika Mkutano wa hadhara wa Wananchi wa Kata ya Sisimba ulioitishwa na Diwani wa Kata hiyo februari,19,2023, Josephine Kamunga katika eneo la wazi,Uhindini,lilipokuwa soko Mjinga lililoteketea kwa moto, baadhi ya wananchi wa Mitaa ya Kata ya Sisimba walisema hawajanufaika na msaada wa Bima ya Afya wakidai kadi zilitolewa kwa upendeleo na wanufaika wa TASAF hawakupendekezwa na mikutano.
“Kinachotokea kwa wananchi waliokosa misaada na waliokosa kunufaika na TASAF watajenga hasira kwa Chama cha Mapinduzi na matokeo yake kitatokea nini katika chaguzi kama hawa viongozi wa chini wameanza kuwabagua wananchi kipindi hiki?,”amesema mmoja wa wananchi wa Kata ya Sisimba.
Akitolea ufafanuzi malalamiko hayo Diwani wa Kata ya Sisimba, Kamunga alisema Mbunge Dk Tulia alitoa msaada huo kwa huruma yake na siyo Serikali na alielekeza wasaidiwe watu wawili katika kila Mtaa ndani ya Kata zote 36 waweze kunufaika.