NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesajili miradi 1,148 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 15.32, iliyozalisha ajira zaidi ya 344,000 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Septemba 2026.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Novemba 2,2026 jijini Dar as Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA Gilead Teri wakati wa Kikao kazi baina yake na Wahariri wa Vyombo vya Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Katika kikao kazi hicho,Teri alianika taarifa ya mafanikio ya TISEZA, iliyohusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika kipindi hicho, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI) ulifikia dola bilioni 9.60, huku uwekezaji wa ndani ukifikia dola bilioni 5.72.
Teri amesema,Mafanikio hayo yametokana na juhudi za mamlaka hiyo katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kuboresha huduma kwa wawekezaji, kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za uwekezaji.
Akizungumzia kuhusu maeneo ya Bagamoyo, Kwala na Nala Mkurugenzi huyo amesema yalipewa kipaumbele katika kuvutia wawekezaji ambapo Mamlaka ilipokea maombi zaidi ya 80 ya matumizi ya ardhi, ambapo 43 yalifikia hatua ya kusainiwa kwa mikataba.
“Maombi hayo yanatarajiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 1.5 na kuzalisha ajira zaidi ya 15,844. Pia, ujenzi wa miundombinu ya Bagamoyo SEZ na maandalizi ya mpango kabambe wa Tanga SEZ yaliendelea.” amesema
Aidha Teri amegusia kuhusu kuboresha huduma kwa wawekezaji
Kupitia Kituo cha Huduma kwa Wawekezaji wa Kimkakati (PISC), wawekezaji 524 walihudumiwa kupitia Premium Lounge.
Amefafanua kuwa kati yao,34 walifanikiwa kusajili kampuni, miradi 83 ilisajiliwa kupitia mifumo husika ya motisha na maeneo ya usindikaji kwa mauzo ya nje, na wawekezaji 142 walipata ushauri kuhusu ardhi, kodi, fursa za uwekezaji na huduma za kifedha.
Kuhusu ufuatiliaji wa miradi ya uwekezaji Teri amejinasibu kuwa
TISEZA ilitoa huduma za baada ya usajili kwa miradi 789, ikizidi lengo la miradi 375. Huduma hizo zilihusisha kutembelea miradi, kufuatilia utekelezaji na kusaidia kutatua changamoto za wawekezaji.
Wakati huo huo ameeleza suala la kuhamasisha uwekezaji wa ndani
Kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, washiriki 1,402 walifikiwa katika maeneo mbalimbali nchini na miradi 24 ilitembelewa na kuhakikiwa.
Amefafanua kuwa Kampeni hiyo ililenga kuongeza uelewa kuhusu fursa za uwekezaji, vivutio vya kodi na ushiriki wa wazalishaji wa ndani katika mnyororo wa thamani.
Katika hatua nyingine Teri ametumia fursa hiyo kuwaalika watanzania wenye maeneo makubwa yanayoweza kukodishwa kwa wawekezaji kufika TISEZA na barua pamoja nakala za umiliki wa maeneo yao ili wapewe miongozo sahihi na kusaidiwa kupata wawekezaji.
“Sisi TISEZA tutamsaidia mwenye eneo linalofaa kukodishwa kwaajili ya uwekezaji baada ya hapo tutamuacha aendelee na mteja wake vile watakavyokubaliana kulingana na mikataba watayoingia” amesisitiza na kuhitimisha Mkurugenzi huyo



