NA MWANDISHI WETU,DODOMA
BODI ya Bima ya Amana (DIB) ipo katika mchakato wa kulipa fidia ya ufilisi awamu ya tatu ya asilimia
30 kwa wadai wa iliyokuwa benki ya FBME walioko Tanzania.
Malipo haya yanafanya wadai wa FBME nchini wawe wamelipwa jumla ya asilimia 85 ya madai yao,
kwani katika awamu ya kwanza na ya pili walilipwa asilimia 30 na asilimia 25, mtawalia.
‘’Kutokana na tathmini iliyofanywa, DIB imeamua kulipa fidia ya ufilisi kwa wadai waliokuwa na amana
zaidi ya shilingi milioni 1,500,000.00 katika benki ya FBME kwa awamu ya tatu kwa upande wa wadai
wa Tanzania pekee,’’ amesema Mkurugenzi Mkuu wa DIB, Isack Kihwili katika taarifa yake.
Aidha,Kamati ya Wadai imeshaidhinisha pendekezo la malipo hayo.
Kwa ujumla, wadai kwa upande wa Tanzania ni 1,414, ambao madai yao ya jumla kwa benki hiyo ni
shilingi bilioni 35.2; wadai wa kimataifa (TIB) wako 866 na madai yao ni shilingi bilioni 308.22.
Pia,
wateja wa tawi la Cyprus ni 5,480 wakidai jumla ya Euro milioni 1,254.62 (sawa na shilingi milioni
3,596.00).
‘’Malipo ya awamu nyingine yatategemea kiasi kitakachokusanywa ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa
fedha zilizozuiliwa na mamlaka ya Marekani (FinCEN),’’ ameeleza Mkurugenzi Mkuu wa DIB na
kuongeza kuwa kuzuiliwa kwa fedha hizo ni moja ya sababu kubwa zilizochelewesha mchakato wa
malipo ya fidia ya ufilisi.
Vilevile, DIB kama mfilisi, itaendelea kufanya tathmini kadri makusanyo yatakavyopatikana na kufanya
malipo ya awamu nyingine kwa wadai pindi yatakapokuwa ya kuridhisha.
Benki Kuu ya Tanzania ilifuta leseni ya Benki ya FBME mwaka 2017 kutokana na kukiuka masharti ya
leseni yake na kuichagua DIB kama Mfilisi.
FBME ilikuwa na makao makuu yake hapa nchini na tawi
nchini Cyprus.
Hii imefanya zoezi la ufilisi kushirikisha mamlaka za Tanzania na Cyprus.

